• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
‘Alcoblow’ kurejeshwa barabarani marekebisho ya sheria yakiidhinishwa

‘Alcoblow’ kurejeshwa barabarani marekebisho ya sheria yakiidhinishwa

Na DAVID MWERE

HUENDA vifaa vya kupima ikiwa madereva wamekunywa pombe wanapoendesha magari, maarufu kama ‘alcoblow’ vikarejeshwa barabarani, ikiwa Bunge la Kitaifa litapitisha marekebisho mapya kwenye Sheria ya Trafiki 2013.

Ni marekebisho yanayotarajiwa kuwa pigo kubwa kwa madereva ambao huwa na uraibu wa kulewa wanapoendesha magari.Marekebisho hayo yamewasilishwa na mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket.Kulingana na mapendekezo ya mswada huo, wale watakaopatikana na hatia watapigwa faini ya Sh100,000, kifungo cha hadi miaka miwili au adhabu zote mbili.

“Mtu yeyote ambaye atajaribu au kupatikana akiendesha gari akiwa mlevi kuliko viwango vinavyohitajika, ataadhibiwa kulingana na sheria,” unaeleza mswada huo.Mapendekezo hayo yanalenga kuboresha sheria ya awali kama ilivyoagizwa na mahakama.

Mnamo 2017, Mahakama ya Rufaa iliitangaza sheria hiyo kuwa marufuku.Bw Kamket alisema mapendekezo yake yanalenga kuiboresha sheria hiyo, ili kuwa katika hali ambapo inaweza kutekelezwa bila pengo lolote.“Marekebisho hayo yatahakikisha ukaguzi wa ikiwa mtu amekunywa pombe utafanywa kwa njia ifaayo kwa kuzingatia taratibu na vipimo vitakavyokuwa wazi kwa kila mmoja,” akasema.

Matumizi ya vifaa hivyo yalisimamishwa mwaka 2017, baada ya kubainika kuwa utekelezaji wake haukulingana na Sheria ya Trafiki. Zoezi hilo lilikuwa likitekelezwa na polisi kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Uchukuzi Barabarani (NTSA).

Majaji GBM Kariuki, Fatuma Sichale na Festus Azangalala wa Mahakama ya Rufaa waliliagiza Bunge kutathmini upya sheria hiyo baada ya mlalamishi kupinga matumizi ya vifaa hivyo.Kabla ya agizo hilo, kifaa hicho kilikuwa kimetumika nchini kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kilianza kutumika mnamo 2014.Sheria hiyo pia inapendekeza utaratibu mpya kuanza kutumika kuwaadhibu wale wanaopatikana wakiendesha magari yao kwa kasi.Inapendekeza anayekiuka sheria hiyo kufungwa gerezani kwa muda wa miezi mitatu, kupigwa faini ya Sh20,000 au kupewa adhabu zote mbili.

You can share this post!

Mdokezi aendelea kumwaga mtama kuhusu mauaji

Familia kusherehekea Krismasi vichakani

T L