• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Jinsi uharibifu wa Milima ya Shella unavyohatarisha Lamu kutorokwa na wakazi

Jinsi uharibifu wa Milima ya Shella unavyohatarisha Lamu kutorokwa na wakazi

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI na wanaharakati wa mazingira, kaunti ya Lamu wameeleza hofu ya uwezekano wa watu wote wa kisiwa cha Lamu wakatoroka miaka ijayo kwa kukosa maji safi ya matumizi.

Hii inatokana na uvamizi na uharibifu mkubwa unaoendelea wa milima ya chemchemi ya maji eneo la Shella ambayo tangu jadi ni tegemeo la kipekee kwa wakazi zaidi ya 30,000 wanaoishi kisiwani Lamu kupata maji safi ya kunywa.

Vyanzo hivyo vya maji eneo la Shella viko kwenye ardhi ya muinuko iliyopanuka kwa zaidi ya kilomita 12 na ukubwa wake mraba ukiwa karibu ekari 2300 na urefu wa juu wa zaidi ya mita 60.

Tangu jadi milima hiyo ya chemichemi ya maji ya Shella imekuwa marufuku kwa makazi ya binadamu katika harakati za kuihifadhi ili kuendelea kutoa maji safi kwa wakazi wa kisiwa cha Lamu.

Miaka ya hivi hivi karibuni aidha, kumeshuhudiwa uvamizi na ujenzi wa makazi ya binadamu kwenye milima hiyo ya vyanzo vya maji Shella, hali inayoaminika kuwa sababu kuu ya uhaba wa kila mara wa maji safi kisiwani Lamu.

Gavana wa Lamu, Issa Timamy kila mara amekuwa akikemea wavamizi wanaoendeleza ujenzi wa majengo yao kwenye milima hiyo ya Shella, akitisha kuwa serikali yake haitasita kuwafurusha wanyakuzi hao wa ardhi.

Bw Timamy amekuwa akionya kuwa endapo wanyakuzi wa ardhi wataachiliwa kuendelea kuvamia, kujenga na hata kuharibu vyanzo vya maji eneo hilo, Lamu basi itaishia kusalia mahame bila mkazi hata mmoja.

Alitaja vyanzo vya maji vya Milima ya Shella kisiwani Lamu, Lake Kenyatta eneo la Mpeketoni na Lake Moa iliyoko tarafa ya Witu kuwa maeneo muhimu yanayostahili kulindwa yasiharibiwe na wanyakuzi.

“Milima ya Shella, Lake Kenyatta na Lake Moa ndizo chemichemi kuu za maji Lamu. Ikiwa kutakuwa na unyakuzi wa kila mara na watu kujenga kwenye Milima ya Shella, eneo kama kisiwa cha Lamu litakosa maji safi kwa matumizi ya binadamu. Hiyo inamaanisha Lamu kutakuwa hakuna maisha tena, ikizingatiwa kuwa maji ni uhai. Mimi kama gavana, sitakubali watu wa Lamu wakose maji kwa sababu ya watu wachache kufaidika. Katu hatutaruhusu watu kuishi kwenye vyanzo hivyo vya maji,” akasema Bw Timamy.

Alisema ofisi yake kwa ushirikiano na Mamlaka ya Udhibiti wa Mazingira nchini (NEMA) imeimarisha vikosi kabambe vya kupiga doria na kuhakikisha vyanzo vya maji Lamu vinalindwa ipasavyo.

“Naweka wazi kwamba yeyote anayetaka kujenga lazima atafute idhini kutoka kwa serikali ya kaunti. Endapo mtu atajenga, hasa kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, ikiwemo Shella, ajue anafanya hayo kwa hasara yake mwenyewe kwani tutamfikia na kubomoa,” akasema Bw Timamy.

Kwa upande wao, wahifadhi wa mazingira walieleza kutamaushwa kwao na jinsi mabwanyenye eneo hilo  wanavyoonyesha kutojali umma na kuendeleza uharibifu wa Milima ya Shella, hivyo kuathiri maji yanayotegemewa na maelfu ya wanakisiwa kutoka eneo hilo.

Afisa Mtendaji wa Shirika la Lamu Marine Forum, Mohamed Athman alitaja kuwa siku za hivi karibuni kisiwa cha Lamu kimeshuhudia maji kukatika ovyo ovyo ilhali yale yapatikanayo yakiwa na kiwango cha juu cha chumvi.

Mwanaharakati wa mazingira wa shirika la Lamu Marine Forum Mohamed Athman akizungumza kuhusu milima ya chemchemi ya maji ya Shella na hofu endapo itaharibiwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

“Zamani Lamu haikukosa maji. Maji yenyewe pia yalikuwa safi kwelikweli. Inasikitisha kwamba miaka ya hivi karibuni eneo hili limekuwa likishuhudia uhaba wa kila mara wa rasilimali hiyo. Wiki haiishi bila ya maji kukatika kisiwani Lamu mara mbili au tatu. Sehemu zingine hata zimeshuhudia maji yakikatika kwa karibu wiki nzima. Maji yakitoka pia ladha yake ni ya chumvi. Haya yote yanatokana na uharibifu wa vyanzo vya maji vya Shella, hasa kutokana na jinsi mabepari wanavyoendeleza ubunifu wa makazi eneo hilo. Lazima hulka hiyo ikome la sivyo Lamu itasalia mahame siku za usoni,” akasema Bw Athman.

Bi Khadija Alwy, ambaye pia ni mwanaharakati wa mazingira kisiwani Lamu, alisema tayari wamekuwa wakiendeleza hamasa kwa jamii kila kuchao kusisitiza haja ya wakazi kuepuka kuvamia na kukalia vyanzo vya maji.

Bi Alwy alisisitiza haja ya ushirikiano wa jamii nzima ya Lamu katika kukinga maeneo muhimu kama vyanzo vya maji kuharibiwa.

Pia aliiomba serikali ya kaunti ya Lamu kwa ushirikiano na serikali kuu kupitia Mamlaka ya uhifadhi wa maeneo na rasilimali za chemichemi (WRMA) kuhakikisha maeneo yote yanayotambuliwa kuwa vyanzo au chemichemi za maji eneo hilo yanatunzwa na kukingwa kupitia ujenzi wa ua maalum.

“Inashangaza kwamba licha ya watu kufahamu kuwa vyanzo vya maji kama vile Milima ya Shella vilivyo muhimu, bado wanavamia nba kuendeleza ujenzi wao. Hatutaki wakazi wafikie kiwango cha kuhama kisiwa cha Lamu sawasawa na ilivyoshuhudiwa miaka zaidi ya 300 iliyopita ya eneo la Takwa kisiwani Manda kuhamwa baada ya maji kugeuka kuwa ya chumvi na maji safi kukosekana kabisa. Tumezidisha hamasa kwa jamii zetu lakini lazima serikali kuchukua hatua kabambe, ikiwemo kuzingira hata kama ni seng’enge kwenye chemichemi za maji ili kuzikinga kutokana na wanyakuzi,” akasema Bi Alwy.

  • Tags

You can share this post!

Wanandoa wanaotaka kupata watoto wakatazwa kula samaki...

Hii hapa siri ya kujipatia ngozi ya kupendeza

T L