• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Mbunge wa UDA afurushwa Kisii akijaribu kusitisha maandamano kwa ahadi ya Sh200 kwa kila mwandamanaji

Mbunge wa UDA afurushwa Kisii akijaribu kusitisha maandamano kwa ahadi ya Sh200 kwa kila mwandamanaji

NA WYCLIFFE NYABERI 

MBUNGE wa Nyaribari Chache, Zaheer Jhanda Jumatano, Julai 19, 2023 alikabiliwa na kibarua kigumu kuwarai raia mjini Kisii kusitisha maandamano kushinikiza serikali kushusha gharama ya maisha.

Muungano wa upinzani, Azimio la Umoja unaendeleza maandamano maeneo mbalimbali nchini, yaliyoitishwa na kinara Raila Odinga.

Bw Jhanda aliwasili mjini humo kwa fujo dakika chache tu baada ya saa sita mchana na kuanza kuyaondoa mawe yaliyokuwa yametumiwa na waandamanaji kufunga baadhi ya barabara.

Kisha alipanda juu ya gari lake kuhutubia waandamanaji waliokuwa wakijihusisha kwenye mchezo wa paka na panya na polisi, lakini mambo yalimwendea mrama alipowakosoa akiwaambia “gharama ya maisha haitapungua kwa kuweka sufuria vichwani,”

Kilichokera raia zaidi, ni kauli ya mbunge huyo wa chama cha UDA aliyedai kuwa ana uwezo kulipa kila mtu aliyekuwa mjini humo Sh200.

Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda alipowasili mjini Kisii kuondoa mawe yaliyoachwa barabarani na raia wakati wa maandamano ya Jumatano, Julai 19, 2023. Picha/WYCLIFFE NYABERI

Matamshhi hayo yalionekana kuwachukiza, wakimtaka aondoke mjini humo mara moja.

“Lazima Ruto aende. Lazima Ruto aende. Tuko njaa. Toka hapa na Sh200 zako,” walisema waandamanaji hao na kumlazimisha Bw Jhanda kukatiza hotuba yake.

Akionekana kughadhabishwa na upokezi alioupata katika eneobunge lake, Bw Jhanda alisema kuwa baadhi ya waandamanaji waliomzomea walikuwa watu wa Nyamira.

“Wengi wenu mnaopiga kelele hata si wa Nyaribari Chache, lakini kwa sababu mimi kama mjumbe niko hapa, nitaangalia mambo yenu,” akasema Jhanda kisha akaondoka.

Maandamano yanazidi kushuhudiwa katika Kaunti ya Kisii huku waandamanaji wakifunga baadhi ya barabara.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wawakamata viongozi wa ODM Kilifi

Wakenya tulieni tuko na ‘plan’, asema Alfred...

T L