• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mhubiri mwingine Kilifi naye atiwa mbaroni sababu msichana wa umri wa miaka 14

Mhubiri mwingine Kilifi naye atiwa mbaroni sababu msichana wa umri wa miaka 14

NA ALEX KALAMA 

MHUBIRI wa kanisa la Jesus Revelation Center (JRC) eneo la Tezo Mbuyuni katika Kaunti ya Kilifi alikamatwa na kufikishwa kwenye kituo cha polisi cha Ngerenya ikidaiwa alikuwa akishiriki ngono na msichana mwenye umri wa miaka 14.

Kulingana na mzee wa Nyumba Kumi eneo la Tezo Macdonald Kenga ni kuwa mhubiri huyo Gilbert Kenga mwenye umri wa miaka 55 amekuwa akishiriki ngono na mtoto huyo ambaye ni muumini wa kanisa lake kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Akizungumza na wanahabari jana Ijumaa, Kenga alisema licha ya familia ya mtoto huyo kumshawishi mhubiri huyo kuachana na mwana wao waliposhuku kuna kitu, na hata baada ya mazungumzo ya kina na mzee wa mtaa huyo, bado juhudi zao hazikufua dafu hali ambayo imesababisha mzee wa mtaa na familia hiyo kupiga ripoti polisi ili mhubiri huyo atiwe mbaroni.

“Alikuwa mshirika kwenye kanisa la mchungaji huyo. Baada ya muda kidogo huyo mtoto alianza kukesha kwenye kanisa pamoja na mchungaji na hilo likaibua maswali zaidi. Familia ya huyo mtoto ilifuatilia na ikaleta hiyo kesi kwangu kama mzee wa Nyumba Kumi,” akasema Mzee Kenga.

Aliongeza kwamba alimuandikia barua mhubiri huyo wakafanya mazungumzo “lakini kumbe aliyapuza yale niliyomwambia.”

“Familia juzi ikafuatilia tena kujaribu kumshawishi aachane na huyo mtoto asilale kwa kanisa ila mchungaji hakusikia,” aliongeza.

Kwa upande wake naibu chifu wa eneo la Majaoni Nzai Katana alieleza kughadhabishwa kwake kwa tendo hilo na kuwataka wakazi katika Kaunti ya Kilifi kutosita kuripoti visa hivyo punde tu vinapotokea katika jamii.

“Mimi nawaambia kwamba wasisite kuripoti hawa wachungaji ambao wana tabia hizo katika jamii yetu kwa sababu tukiangalia katika nyumba za kuabudu ni mahali ambapo pako na hadhi kubwa sana katika jamii yetu lakini unakuta siku hizi hapo ndio mahali ambapo wanajificha watu ambao wanapotosha jamii. Kwa hivyo ningependa mtu yeyote anayejua wanaojificha kwa dini kufanya maovu katika jamii aripoti katika ofisi zetu na hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Bw Nzai.

Mtoto huyo alipelekwa katika hospitali kuu ya Kilifi kufanyiwa uchunguzi wa kina.

“Yalianza kitambo mpaka sasa hivi tumepatiwa huyo mtoto apelekwe kwa daktari apimwe halafu turejee kwa kituo cha polisi na hayo majibu ya daktari halafu huyo mshukiwa apelekwe mahakamani,” alisema.

Lakini mhubiri huyo naye jana Ijumaa alipofikishwa katika Mahakama ya Kilifi Mjini, aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

  • Tags

You can share this post!

Rovanpera, Ogier waingia Safari Rally

Sudan: Amerika yatishia kuweka vikwazo vipya

T L