• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Mung’aro aahidi kuboresha huduma za afya mashinani 

Mung’aro aahidi kuboresha huduma za afya mashinani 

Na ALEX KALAMA 

GAVANA wa Kilifi Gideon Mung’aro amewahakikishia wakazi wa kaunti yake kwamba serikali yake itaboresha huduma za afya katika hospitali zote za umma, ikiwemo zahanati za mashinani.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi Mung’aro alisema ataweka mikakati maalum na ya kisheria kuanza kuwalipa wahudumu wa afya nyanjani.

“Kwa sasa mikakati ya kisheria inaendelea kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya nyanjani wanapata ruzuku, ili kuendeleza majukumu yao ya kuhudumia jamii,” alisema gavana Mung’aro.

Hata hivyo, alisema licha ya mipango ya serikali ya kitaifa kutoa ruzuku ya Sh2, 500 kwa wahudumu, Kaunti ya Kilifi inalenga kuhakikisha kuwa imeboresha afya kwa wakazi kwa kuwajali wahudumu wa afya nyanjani.

Kauli yake ilipigwa jeki na mwakilishi wa wadi ya Shella mjini Malindi, Twaher Abdhulkarim aliyesisitiza haja ya serikali ya kaunti hiyo kulinda afya ya wakazi kwa kuboresha miundo msingi ya hospitali za mashinani.

“Tunajua wewe ni mchapakazi lakini nataka nikujulishe kwamba hospitali nyingi za mashinani bado zinakumbwa na changamoto ya uhaba wa madaktari, ilhali zingine hazina vifaa. Tunakuomba usaidie kuimarisha maisha ya wanajamii Kilifi,” alisema Bw Abdhulkarim.

Aidha, kiongozi huyo alidokeza kuwa mikakati inaendelea itakayohakikisha wahudumu wa afya ya nyanjani kaunti nzima wanapata ruzuku kutoka kwa serikali kuu.

  • Tags

You can share this post!

KMJA yaeleza hofu baada ya afisa wa mahakama kuuawa kwa...

Wananchi kuwa na usemi mkuu katika biashara ya pombe

T L