• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Ndovu mkorofi Taita Taveta anayebomoa nyumba za watu na kula unga   

Ndovu mkorofi Taita Taveta anayebomoa nyumba za watu na kula unga  

NA LUCY MKANYIKA

KATIKA Kijiji cha Zongwani Sagalla, Kaunti ya Taita Taveta, wakazi wamempa ndovu mmoja jina ‘maunga,’ kwa sababu ya uzoefu wake kubomoa nyumba ili kula unga wa mahindi.

Tembo huyu amekuwa maarufu kwa ukorofi wa kuvunja nyumba haswa wakati wa usiku ili kula unga tu na hivyo kuhatarisha maisha ya wenyeji.

Wenyeji waliozungumza na Taifa Leo Dijitali walisema kuwa kati ya kundi la ndovu linalozunguka eneo hilo, ndovu huyo amekuwa na hamu na tabia ya kula unga kila anapovunja nyumba.

Bw Anderson Keke, mzee wa mtaa eneo hilo alisimulia kuwa tembo huyo hung’oa paa la nyumba kwa kutumia mkonga wake mrefu na kisha kutafuna unga.

“Ikiwa unga uko kwa pakiti au gunia dogo basi huula mzima mzima. Ikiwa uko kwenye gunia kubwa huumwaga na kuuramba,” akasema.

Bw Keke alisema vilevile ndovu huyo huvamia vijiji vya Marapu na Rahasi ambapo hufanya uharibifu mkubwa na kuacha wenyeji na hofu ya maisha yao.

Bw Keke alisema kuwa wiki iliyopita uvamiz uliongezeka, jambo ambalo limesababissha wakazi kuishi kwa hofu.

Kufikia sasa, tangu mwaka jana, 2022 zaidi ya nyumba 30 zimevamiwa na ndovu huyo.

“Wiki hii pekee nyumba tatu zimevamiwa,” Bw Keke alidokeza.

Alisema uvamizi wa tembo hao umesababisha kero na matatizo ya kifedha kwa wanakijiji na kuongeza matukio ya migogoro ya binadamu na wanyamapori katika eneo hilo.

Mnamo Jumatano usiku (Oktoba 30, 2023), ndovu huyo mtundu alivamia nyumba ya Bi Rhoda Mwakireti na kung’oa paa na kula unga wa mahindi wa kilo 5, nafaka ya mahindi ya kilo 10, mboga zilizokaushwa na mbaazi.

Bi Mwakireti hakuwa nyumbani wakati kisa hicho kilipotokea.

“Nilikuwa hospitalini na mama yangu mgonjwa. Nilipigiwa simu na majirani wakanijulisha kuhusu tukio hilo. Namshukuru Mungu sikuwepo nyumbani usiku huo,” alielezea.

Hii si mara ya kwanza ndovu huyo kuvamia nyumba yake. Mei 2023, tembo huyo alivunja nyumba ya mtoto wake na kubomoa sehemu ya ukuta na paa.

“Hadi leo hatujapata pesa ya kurekebisha hiyo nyumba ya kwanza. Sijui sasa hata hii nitarekebisha vipi,” alisema.

Mkazi mwingine, Jemimah Mwakio anasema mwezi uliopita (Oktoba) ndovu huyo alivamia nyumbani kwake.

“Aliondoa paa na kula gunia la mboga zilizokaushwa. Nimeripoti kwa Shirika la Wanyamapori (KWS) lakini sijapokea msaada wowote,” alisema.

Alisema tukio hilo limewashangaza wenyeji kwani si la kawaida.

“Nilipokuwa mdogo tulikuwa tunaona ndovu wakiingia shambani na kuharibu mimea lakini hii ni mara ya kwanza wameanza kuvamia nyumba,” alisema.

Mwakilishi wa wadi ya Sagalla Bryson Mwambi alisema atawasiliana na shirika la KWS kuona jinsi wanyamapori hao watafurushwa kutoka eneo hilo.

“Nitazuru afisi za KWS ili kuwafahamisha kuhusu tishio hili,” aliahidi.

Kaunti ya Taita Taveta kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na visa vya mizozo kati ya binadamu na wanyamapori, huku ndovu wengi kutoka mbuga jirani ya Tsavo wakivamia makazi ya watu mara kwa mara.

Matukio kama haya mara nyingi hutokea katika maeneo mengi ya kaunti hiyo kutokana na ukaribu wao na mbuga hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Tuache kurushiana lawama tunapopigana na Al-Shabaab, Duale...

Wanafunzi wa vyuo vikuu wanavyolala njaa kwa kucheleweshewa...

T L