• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Tuache kurushiana lawama tunapopigana na Al-Shabaab, Duale ashauri

Tuache kurushiana lawama tunapopigana na Al-Shabaab, Duale ashauri

NA KALUME KAZUNGU

RAIS William Ruto, Naibu wake Rigathi Gachagua na Waziri wa Ulinzi Aden Duale wametangaza vita vikali dhidi ya Al-Shabaab ambao wamekuwa wakihangaisha Lamu na kaunti nyingine za Kaskazini mwa Kenya, wakiwataka magaidi hao kujua ujanja wao umefika kikomo. 

Wakihutubia umma katika kisiwa cha Kizingitini huko Lamu Mashariki wakati wa ziara ya kuzindua miradi ya maendeleo, viongozi hao walieleza kukerwa kwao na hulka ya magaidi kupenya nchini, kuvamia na hata  kuua wananchi wasio na hatia na kuharibu mali.

Kati ya Juni na Septemba mwaka huu, vijiji, hasa vile vya Lamu Magharibi na vichache vya Lamu Mashariki vimeshuhudia uvamizi wa Al-Shabaab, ambapo watu zaidi ya 30, ikiwemo walinda usalama na raia wameuawa ilhali nyumba zaidi ya 20 na kanisa vikiteketezwa na magaidi hao.

Baadhi ya vijiji vilivyoshuhudia mashambulizi hayo ni Juhudi, Salama, Widho, Marafa, Ukumbi, Mashogoni, Nyongoro, Lango la Simba, Pandanguo na Mlima Faru, vyote vikipatikana Lamu Magharibi ilhali vile vya Lamu Mashariki ni pamoja na Bodhei, Baure, Mararani, Sarira, Milimani na viungani mwake.

Kwenye hotuba yake, Rais Ruto alishikilia kuwa utawala wake katu hautaruhusu magaidi kuendelea kutawala nchini, akitaja kuwa tayari amezungumza na mawaziri, hasa wale wanaohusiana na usalama wa ndani na ulinzi wan chi kuona kwamba vita dhidi ya Al-Shabaab vinazidishwa nguvu.

“Nataka kuweka wazi kwamba wale magaidi wanaojidai kuhangaisha Lamu mjue tutapambana na nyinyi. Hatuwezi kuruhusu wahalifu na magaidi waje kujenga kibanda hapa. Na ndio sababu tumekubaliana na mawaziri kwamba magaidi lazima watoke hii Lamu, na wasipotoka tutapambana na wao . Mambo ya magaidi hapa aidha watoke Kenya ama wasafiri waende mbinguni,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliwasihi wananchi wa Lamu na viongozi kuepuka kugawanywa na magaidi na badala yake waungane kumpiga na kumshinda adui huyo.

“Mambo ya usalama ningependa kushauri hivi. Viongozi hapa mko na jukumu la kuwazungumzia wananchi kwa njia inayofaa ili baadaye isije kubadilika kuwa uchochezi na kuleta uhasama kati ya jamii, makabila na dini,” akasema Dkt Gachagua.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi, Aden Duale aliwasisitizia viongozi wa Lamu na wananchi kuungana na kumtambua adui mmoja anayefaa kumalizwa ambaye ni Al-Shabaab.

Bw Duale alisema serikali iko chonjo kumpiga Al-Shabaab ndani ya Somalia na pia kwenye mpaka wa Kenya nan chi hiyo jirani.

Waziri huyo wa Ulinzi hata hivyo aliwaonya wale wanaoshirikiana na magaidi kutekeleza uvamizi Lamu, akisema siku zao zimehesabiwa.

Bw Duale hata hivyo alitaja kuwa ziara zake za kila mara Lamu, ambapo amekuwa akikutana na kujadiliana na viongozi na wananchi zimezaa matunda kwani idadi ya visa vya mashambulio ya magaidi vimepungua pakubwa eneo hilo siku za hivi karibuni.

“Nawashukuru nyinyi viongozi na wananchi hapa Lamu. Ujio wangu wa kila mara hapa naona tayari umezaa matunda. Tuko chonjo. Ukikadiria utapata kuwa ni majuma mengi yamepita bila kushuhudia mashambulio ya Al-Shabaab. Tuzidi kushirikiana na kuepuka kunyosheana vidole vya lawama. Tujue kwamba tunamwinda na kumkabili adui mmoja dhidi yetu ambaye ni Al-Shabaab na tutamshinda,” akasema Bw Duale.

Naye Gavana wa Lamu, Issa Timamy, aliishukuru serikali kuu, kupitia Wizara za Ulinzi na ile ya Usalama wa Ndani kwa kuhakikisha utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi Lamu unakabiliwa vilivyo na kupunguzwa.

“Twashukuru serikali kuu na maafisa wetu wa usalama, wakiwemo wanajeshi (KDF) kwa juhudi zao katika kuhakikisha Lamu iko na amani. Tutazidi kushirikiana kuhakikisha Lamu na nchi nzima kwa ujumla ni tulivu ili maendeleo yaafikiwe ipasavyo,” akasema Bw Timamy.

  • Tags

You can share this post!

Mark Zuckerberg auguza jeraha la goti akijiandaa kushiriki...

Ndovu mkorofi Taita Taveta anayebomoa nyumba za watu na...

T L