• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Polisi walioua bila kukusudia jela miaka 48

Polisi walioua bila kukusudia jela miaka 48

PHILIP MUYANGA na MASHIRIKA

MAAFISA watatu wa polisi pamoja na mwenzao aliyestaafu, Jumatatu walihukumiwa kifungo cha miaka 48 kwa jumla kwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua raia wa Uingereza.

Jaji Eric Ogola alimhukumu Naftali Chege miaka 15 gerezani, Charles Wang’ombe miaka 12, Ismael Baraka miaka tisa na John Pamba miaka 12.

Wana siku 14 kukata rufaa.

John Pamba, Chege, Wang’ombe Munyiri (aliyestaafu) na Bulima walikuwa wameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa mauaji ya Alexander Monson, alipokuwa kizuizini.

Kisa hicho kilitokea Mei 19, 2012 katika eneo la Diani, eneobunge la Msambweni, Kaunti ya Kwale.

Akitoa uamuzi wake jana, Jaji Erick Ogola alisema mahakama ilithibitisha kuwa marehemu aliteswa kwa kupigwa na watu wasiojulikana alipokuwa kizuizini katika kituo cha polisi.

Mahama ilisema uamuzi huo ulitolewa kwa vile ni vigumu kubainisha wazi ni nani hasa alihusika katika mauaji kwa vile polisi wameficha mambo mengi.

Mapema mwaka huu, Jaji Ogola alipata wanne hao walikuwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi dhidi yao.

“Washtakiwa wana jukumu la kuambia mahakama hii kilichotokea usiku wa kisa hicho,” Jaji Ogola alisema wakati huo.

Alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulibainisha kuwa Monson alikuwa buheri wa afya wakati alipokamatwa.

Mahakama iliongeza kuwa, ushahidi pia ulionyesha washtakiwa ndio walimhudumia alipopelekwa kizuizini.

Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Bw Alexander Muteti, alikuwa ameambia mahakama kuwa, washtakiwa ni maafisa wa polisi ambao wamepokea mafunzo kuhusu matumizi ya silaha na ujasusi.

“Suala hili linahusu uadilifu wa kitaifa wa mfumo wetu wa haki. Marehemu hakuwa Mkenya,” aliambia mahakama.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeita mashahidi 32 akiwemo mamake marehemu, na afisa wa upelelezi kutoka kwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA).

Afisa wa polisi aliyemkamata Monson, Bw William Serem, aliambia mahakama kuwa mshukiwa huyo na mwenzake walifikishwa katika kituo cha polisi cha Diani akiwa buheri wa afya.

Shahidi huyo aliambia mahakama kuwa hali ya Monson ilionekana kuwa shwari alipokamatwa kwani hata alimtetea mwenzake aliyekamatwa pamoja naye na kuwaomba polisi wamwachilie huru huku akiwaeleza kuwa yeye ndiye alishikwa akivuta bangi.

Bw Kennedy Mutai, aliyekuwa katika ofisi ya kusajili washukiwa katika ushahidi wake alisema kuwa alipofika kazini asubuhi iliyofuata alimwona Monson sakafuni akionekana kutatizika.

Aliongeza kuwa mshukiwa huyo alipomwona alijaribu kuinua mkono kama ishara ya kuomba msaada.

Mipango ilifanya na Bw Monson alipelekwa katika hospitali ya kibinafsi lakini alifariki akipokea matibabu.

You can share this post!

Mwendwa aachiliwa kwa dhamana ya Sh4Milioni pesa taslimu

Diwani wa Landimawe aafikiana na Nairobi Water kusambaza...

T L