• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Diwani wa Landimawe aafikiana na Nairobi Water kusambaza maji Mukuru-Kayaba

Diwani wa Landimawe aafikiana na Nairobi Water kusambaza maji Mukuru-Kayaba

Na SAMMY KIMATU

DIWANI wa Landimawe katika kaunti ndogo ya Starehe, Bw Herman Azangu amewahakikishia wakazi wa mtaa wa mabanda wa Kayaba kwamba watapata maji safi wakati wowote kuanzia wiki hii.

Aidha, alitamka hayo jana baada ya kuandaa kikao na usimamizi wa kampuni ya kusambaza maji katika kaunti ya Nairobi (Nairobi Water Company) katika makao makuu ya kampuni yalioko kwenye Eneo la Viwanda.

Maelfu ya wakazi wamehangaika kwa zaidi ya wiki tatu bila maji baada ya kampuni hilo kuondoa mita za maji ili kupisha nafasi kwa ujenzi wa barabara mtaani humo.

Kwa mujibu wa Bw Azangu, mwanakandarasi ameanza rasmi mradi wa ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha barabara ya Entreprise na barabara ya Aoko kupitia mtaani humo.

“Wahandisi wa Nairobi Water waliondoa mita zao ili wapeane nafasi ya ujenzi wa barabara. Baada ya kufanya kikao na usimamizi wa kampuni hiyo tumeafikiana wakazi wa Kayaba watapeana sehemu watakazowekewa mita za maji ili wasambaziwe maji na hali irudi na kuwa ya kawaida,” Bw Azangu akasema.

Diwani wa Landimawe katika kaunti ndogo ya Starehe, Bw Herman Azangu. Picha/ Sammy Kimatu

Fauka ya hayo, wakazi walikuwa wakiamka usiku kuchota maji kutoka bomba zinazosambaza maji kutoka mtaa jirani wa mabanda wa Maasai.

Wlkati wa usiku vurumai na fujo zimeripotiwa huku watu wakipigania maji ambapo wengine walipatikana wamekata paipu za wenyewe na kuchota maji bila kulipa.

“Ili kuzuia maafa kutokana na mzozo wa maji, nimechukua hatua ya haraka na kushukuru Nairobi Water kwa kukubaliana kwamba watawapatia wakazi wa mtaa wa manbanda maji tena,” akanena.

Vilevile, mwanasiasa huyo laiwaomba wakazi kulinda mita zinazowekwa, mifereji sawia na maji akisema ni bidhaa muhimu kwa kila mkazi mtaani.

Awali, wakazi walitegemea maji kutoka kisima kilichochimbwa ndani ya Shule ya Msingi ya Sancta Maria-Mukuru.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo walisema japo maji ya kisima yapo, yana ladha ya chumvi na hawanywi bali wanayatumia tu katika kufanya usafi wa nyumbani.

“Tulishauriwa tusinywe maji ya kisima moja kwa moja kwa sababu za kiafya. Hata hivyo, maji hayo hutumika kwa kufulia nguo na kupiga deki,” Bi Jane Mbula Peter, mhudumu wa afya mtaani, akasema.

Bi Jane aliongeza kwamba sababu nyingine ya ukosefu wa maji mtaani ulitokana na kuharibika kwa mashine ya kupiga maji katika mradi wa kisima.

“Pampu ya kupiga maji katika shule ya Mukuru iliharibika na mradi ukasimama. Wakazi walihangaika kwa kukosa maji yanayosambazwa na kampuni ya Nairobi Water na kulazimika kutembea mbali hadi mtaa wa mabanda wa Maasai,” Bi Regina Nzomo, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Sancta Maria Mukuru akanena.

You can share this post!

Polisi walioua bila kukusudia jela miaka 48

Vita Ethiopia vyatishia hali ya Kenya

T L