• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Sakaja atabasamu madiwani wa UDA wakiunga mkono ‘Dishi na County’ inayopigwa vita na Azimio

Sakaja atabasamu madiwani wa UDA wakiunga mkono ‘Dishi na County’ inayopigwa vita na Azimio

NA WINNIE ONYANDO

MADIWANI wa United Democratic Alliance (UDA) katika Kaunti ya Nairobi wamemtetea Gavana Johnson Sakaja dhidi ya malalamishi kuhusu utekelezaji wa programu ya lishe shuleni almaarufu ‘Dishi na County’.

Wakiongozwa na diwani wa Mutiini, Martin Mwangi, madiwani hao walisema Jumanne kwamba mpango huo wa gavana Johnson Sakaja unapigwa vita kisiasa.

“Tuko hapa kuwakashifu wale wanaopinga miradi ya gavana Sakaja. Gavana anajaribu sana kuhakikisha kuwa watoto wetu wanakula shuleni. Hakuna haja ya kumpinga,” akasema Bw Mwangi.

Programu hiyo ya gavana Sakaja imekuwa ikikashifiwa huku baadhi ya watu wakitilia shaka utekelezaji wake. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alidai wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Tumaini hawakuwa wakipata chakula hicho licha ya kwamba walikuwa wametimiza masharti.

Hata hivyo, gavana huyo alikanusha madai kuwa serikali yake imeshindwa kutekeleza programu hiyo.

Katika taarifa kupitia mtandao wa kijamii ya X (Twitter), Sakaja alidai kuwa watu wanaopinga mpango huo wana nia fiche.

“Hakuna haja kuendeleza propaganda. Kadhalika, hakuna haja kuwatumia watoto kuendeleza ajenda za kisiasa. Shule ambazo zilikuwa katika orodha ya awamu ya kwanza zimekuwa zikipokea chakula kila siku bila kuchelewa. Tayari, watoto 80,000 wanapata chakula chini ya programu hiyo,” Sakaja alisema.

  • Tags

You can share this post!

Al-Shabaab waua mwanamume kwa kukataa kuwaonyesha vituo vya...

Bilionea aliyeanzisha Equity Bank apigwa mnada

T L