• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Serikali iharakishe miradi ya Italia – Kingi

Serikali iharakishe miradi ya Italia – Kingi

Na MAUREEN ONGALA

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi, ameomba serikali ya kitaifa iharakishe kuidhinisha maelewano na serikali ya Italia, kuhusu ufadhili wa miradi ya mamilioni ya pesa eneo la Pwani.

Akizungumza alipokutana na balozi wa Italia humu nchini, Bw Alberto Pieri, gavana huyo alisema miradi inayohitaji kutekelezwa kupitia kwa maelewano hayo, itasaidia kuharakisha ustawi wa uchumi uliopata pigo janga la corona lilipotua.

“Imekuwa desturi kwa serikali ya Italia kusaidia Kilifi kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile uimarishaji wa miundomsingi, uwekezaji, utalii na utumizi bora wa rasilimali za baharini,” akasema.

Bw Pieri alikuwa amezuru Malindi kuhudhuria Tamasha la Mapishi ya Kiitaliano ambalo hufanyika kila mwaka kwa kipindi cha wiki nzima.

Alifichua kuwa serikali yake na Kenya ziko katika harakati za mwisho za kuidhinisha fedha zitakazotolewa ili kuwekezwa katika sekta ya baharini na miundomsingi Pwani.

“Tuliwasilisha orodha ya miradi ambayo inatilia maanani ustawi wa rasilimali za baharini ili kusaidia kuinua sekta ya uvuvi na nyinginezo zinazotegemea bahari. Kuna miradi mingine mingi tunalenga Pwani,” akaongeza.

Wakati huo huo, Balozi alipongeza mikakati ambayo serikali imeweka kukabiliana na ueneaji wa maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema mikakati kama vile kusambaza chanjo kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya nchi itasaidia kupunguza maambukizi zaidi.

Bw Kingi alisema serikali ya kaunti pia imeweka mipango ya kutosha kuhakikisha kuwa wadau katika sekta ya utalii wanaepusha usambazaji wa virusi hivyo, kama vile kuwapa wahudumu wa hoteli kipaumbele katika kupokea chanjo ya kuepusha Covid-19.

You can share this post!

Riziki: Wamlilia Ruto awatoe kwa ukahaba

Wageni Pwani waonywa kuwa makini baharini

T L