• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Soko jipya la Makongeni mjini Thika kugharimu Sh400 milioni

Soko jipya la Makongeni mjini Thika kugharimu Sh400 milioni

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Makongeni mjini Thika watanufaika na ujenzi wa soko la kisasa ili wachuuzi wa vyakula wafaidike.

Mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a alisema tayari serikali kuu imetenga takribani Sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.

Mnamo mwaka wa 2015 soko hilo liliweza kuchomeka huku  mamilioni ya fedha yakiangamia.

“Kwa hivyo wachuuzi wengi wa vyakula wamepata pigo kubwa huku wakikosa mahali maalum pa kuuzia bidhaa zao,” alisema mbunge huyo.

Kulingana na mbunge huyo, iwapo soko hilo litakamilika bila shaka wachuuzi na wafanyabiashara wapatao 5,000 watapata nafasi ya kuendesha biashara zao.

“Mimi kama mbunge wenu nimekuja hapa Makongeni kuona ya kwamba matakwa yenu tanaangaziwa haraka. Nimekuwa mukiteseka kwa muda mrefu,” alisema mbunge huyo.

Kulingana na mpango uliopo, iwapo mradi huo wa soko utakamilika kutakuwepo na maeneo ya kuegesha magari, vibanda vya kisasa vya kuuzia vyakula, mabomba ya majitaka yatarejebishwa, kutakuwa na sehemu ya wanawake kunyonyeshea watoto wao, na pia mahali pa watoto wadogo kuchezea wakati wazazi wao wanaendelea na biashara.

Kulingana na mbunge huyo, wakati wa ukarabati wa soko hilo wachuuzi hao watapelekwa katika eneo la Annas karibu na duka la jumla lililoko karibu na kituo cha magari cha Makongeni mjini Thika.

Alisema serikali kuu pia ina mipango ya kujenga masoko mengine katika maeneo ya Kiandutu, Ngoliba, na Gatuanyaga.

“Tunataka kuona wananchi popote walipo wakiendesha biashara yao bila wasiwasi wowote. Hatutaki kusikia malamiko tena,” alisema mbunge huyo.

Mwakilishi wadi (MCA) wa Kamenu mjini Thika Bw Peter Mburu alisema yeye yuko tayari kufanya kazi na viongozi wote mradi tu ni kwa ajili ya wananchi.

“Sisi mlituchagua tuwatumikie kama viongozi na kwa hivyo mbunge wetu Bi Ng’ang’a na mimi tutafanya juhudi kuona ya kwamba mradi huu wa soko unafanikiwa,” alisema Bw Mburu.

Alisema soko la Makongeni linavutia wafanyabiashara na wateja wengi kutoka Kiambu, Murang’a, Garissa na hata Machakos.

Kiongozi huyo alitaka serikali kuu kuungana na ile ya kaunti kuona ya kwamba wakazi wa Makongeni wanapata soko la kisasa.

“Kile tungetaka kuona ni soko limejengwa na wananchi waendelee na biashara zao,” alisema mwakilishi huyo wa wadi.

  • Tags

You can share this post!

Etale asema mlinzi wa Raila ameachiliwa huru

Janet Okello: Kenya Lionesses ina kibarua kigumu kuingia...

T L