• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Tumetokomeza kipindupindu, endeleeni na shughuli zenu, Nakhumicha aambia watu wa Lamu

Tumetokomeza kipindupindu, endeleeni na shughuli zenu, Nakhumicha aambia watu wa Lamu

NA KALUME KAZUNGU

WAZIRI wa Afya Susan Nakhumicha amewataka wakazi wa Lamu na wananchi kwa ujumla kuondoa hofu kuhusiana na mlipuko wa kipindupindu ambao umeshuhudiwa kwenye kaunti hiyo kwa karibu wiki tatu sasa, akisema idara yake imedhibiti hali vilivyo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutathmini hali ya afya, hasa visa vya maradhi ya kipindupindu na changamoto ya mafuriko Kaunti ya Lamu Jumatano, Bi Nakhumicha aliweka wazi kuwa kati ya visa 113 vya kipindupindu viliyotangazwa Lamu, ni 63 pekee ambavyo hadi sasa vimethibitishwa.

Alisema kati ya kesi 63 hizo, ni kesi 5 pekee zilizohusisha wagonjwa wa kipindupindu kulazwa ilhali kesi nyingine zikiwa ni zile za waathiriwa kutibiwa na kwenda nyumbani.

Wakati wa ziara ya Jumatano, Bi Nakhumicha alikabidhi kaunti vifaa vya kimatibabu vitakavyosaidia wahudumu wa afya kuwashughulikia vilivyo wagonjwa wa kipindupindu eneo hilo.

“Tumefika hapa kuwahakikishia wakazi wa Lamu kwamba tuko nanyi kukabiliana na hizi changamoto za mafuriko na pia kipindupindu hapa. Msiwe na shaka.Tumedhibiti vilivyo kipindupindu na hii ndiyo sababu kati ya kesi 63 za kipindupindu zilizothibitishwa eneo hilo, ni wagonjwa watano pekee ambao wamelazwa hospitalini hadi sasa. Tutashirikiana kuangamiza kabisa kipindupindu eneo hili,” akasema Bi Nakhumicha.

Akigusia athari za mafuriko, Waziri huyo Wa Afya alisema serikali kuu itaendeleza kushirikiana na kaunti zote hapa nchini kukabiliana na hali hiyo.

Katika kaunti ya Lamu, Bi Nakhumicha alitangaza kufikisha madawa na vifaa vingine vya kimatibabu vya kukabiliana na mafuriko vilivyogharimu serikali kuu kima cha Sh6 milioni.

“Tunafahamu familia nyingi zimeathiriwa na mafuriko eneo hili. Tumeleta vyandarua 6,000 vya kusaidia waathiriwa wa mafuriko Lamu kujikinga dhidi ya mbu. Pia tumesambaza chakula cha msaada. Tutazidi kusimama nanyi katika kukabili kipindupindu na athari nyingine nyingi zinazoletwa na mvua kubwa inayonyesha kote nchini,” akasema Bi Nakhumicha.

Wakati wa ziara hiyo, Bi Nakhumicha pia aliandamana na msemaji wa serikali, Bw Isaac Mwaura ambaye alimsifu Gavana wa Lamu, Issa Timamy kwa juhudi zake kuhakikisha kuna miundomsingi bora, hasa ya kimatibabu kwa wakazi.

Akigusia suala la athari za El Nino, Bw Mwaura alitaja kaunti za Taita Taveta, Migori na Meru kuwa zenye kuathirika zaidi na mafuriko.

Bw Mwaura pia alitaja Lamu na Tana River kuwa maeneo ambayo huenda yakaingia kwenye orodha ya kaunti zilizoathiriwa zaidi na mafuriko yanayoendelea nchini.

Kulingana na Bw Mwaura, mafuriko yameharibu miundomsingi muhimu Lamu, ambapo ekari 832 za mimea, maboma 23 ambayo ni makazi ya binadamu, vivuko vitatu, shule tatu na ofisi ya chifu eneo hilo la Lamu vimesombwa na mafuriko.

Alitaja shule za msingi za Rehema, Faza na Safirisi ambazo miundomsingi yake imeharibika na mafuriko.

“Serikali kwa ushirikiano na mashirika ya misaada ya kibinadamu tayari inafanya kila jitihada kuwafikia waathiriwa wa mafuriko popote walipo Lamu. Pia tunasambaza dawa, vyakula na hata kuwasaidia watunkuhamia maeneo salama huko Moa, Lamu,” akasema Bw Mwaura.

Gavana wa Lamu Issa Timamy aliishukuru serikali kuu kwa jitihada zake kuzisaidia kaunti kukabiliana na kipindupindu na pia mafuriko.

“Tayari tumetambua familia zipatazo 10,000 zilizoathiriwa Vibaya na mafuriko. Tutashirikiana na serikali kuu na wahisani wengine ili tuwafikie na kuwasaidia kwa matibabu na kiwasambazia chakula hapa Lamu,” akasema Bw Timamy.

  • Tags

You can share this post!

Mama mboga aliyedunga kisu mgeni aliyemvamia nyumbani...

Ripoti ya matibabu yafichua ‘njama’ katika uchunguzi wa...

T L