• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Ripoti ya matibabu yafichua ‘njama’ katika uchunguzi wa kesi ya unajisi

Ripoti ya matibabu yafichua ‘njama’ katika uchunguzi wa kesi ya unajisi

NA BRIAN OCHARO

RIPOTI ya matibabu imefichua jinsi uchunguzi wa waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono katika vituo vya matibabu unavyoweza kutumiwa vibaya kwa faida za kibinafsi.

Uchunguzi wa tatu uliofanyiwa msichana wa miaka tisa ambaye alidaiwa kunajisiwa sasa unafafanua kuwa mtoto huyo hajanajisiwa.

Hii inapingana na ripoti ya awali ambayo ilikuwa imetoa matokeo chanya ya unajisi. Uchunguzi huo wa tatu wa matibabu ulifanywa na madaktari wanne.

“Mtoto huyo yuko sawa. Hakuna michubuko wala makovu yaliyoonekana,” ripoti hiyo iliyotiwa saini na madaktari watatu na muuguzi anayesimamia Kituo cha waathiriwa wa Unyanyasaji wa Kijinsia katika hospitali kuu ya eneo la Pwani (CGTRH), ambapo uchunguzi huo ulifanyika ilisema.

Uchunguzi huo wa tatu ulifanyika mbele ya watu 10, ikiwa ni pamoja na madaktari watu, muuguzi mmoja, afisa wa watoto, na mama wa mtoto huyo.

Ripoti hii inakinzana na ripoti ya awali kutoka kituo hicho kimoja iliyothibitisha kuwa msichana huyo alinajisiwa.

Ripoti hiyo ambao sasa imewasilishwa kortini, iliamriwa na Mahakama Kuu mjini Mombasa kutokana na ripoti zinazokinzana za uchunguzi wa awali.

Mahakama Kuu ilipokea taarifa za fomu mbili zinazokinzana za Huduma ya Baada ya Ubakaji (PRC), moja ikionyesha kuwa mtoto huyo alinajisiwa huku ingine ikitoa matokeo tofauti ilisababisha wasiwasi kuwa taratibu za matibabu zilikuwa zikichezewa ili kufikia matokeo mahususi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Olga Sewe alitoa agizo kwa mtoto huyo kufanyiwa uchuguzi wa matibabu kwa mara ya tatu ili kubaini ukweli, baada ya ripoti mbili zinazokinzana kutolewa kutokana na uchunguzi huo wa kimatibabu.

Uchunguzi huo wa tatu ambao kwa sasa umeondoa shauku juu ya madai ya unajisi wa mtoto huyo uliamriwa kufanywa na daktari wa uzazi na mshauri wa magonjwa ya wanawake katika CGTRH, mbele ya matabibu wawili ambao walitayarisha ripoti zinazokinzana, pamoja na wazazi au walezi wa mtoto huyo.

Kesi hiyo ilifika Mahakama Kuu baada ya shirika la kutetea haki za binadamu Commission for Human Rights and Justice (CHRJ) kuomba kufutwa kwa fomu mbili za awali za PRC zenye matokeo yanayokinzana, zikitaja nia mbaya kwa mmoja wa wahusika waliokuwa wakishinikiza madai ya unajisi wa mtoto huyo.

Mkurugenzi mtendaji wa CHRJ Julius Ogogoh alimweleza Jaji Sewe kwamba mojawapo ya ripoti hizo inaonekana kubadilishwa kwa nia mbaya, hivyo basi mahakama ilihitaji kuwa wazi kuhusu hali ya mtoto huyo.

Baba mzazi wa mtoto huyo aliaga dunia kabla ya kuzaliwa kwake. Baadaye, mamake aliingia katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine, ambaye sasa ni baba wa kambo wa mtoto huyo.

Mtoto huyo alipelekwa hospitali kuchunguzwa baada ya kudaiwa kuwa alionekana kuwa alinajisiwa.

Mtoto huyo alipelekwa hadi CGTRH kwa uchunguzi, na fomu ya PRC ilionyesha kuwa alinajisiwa.

Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa mtoto huyo alipekwa katika Hospitali ya Pandya kwa uchunguzi ambapo daktari alithibitisha kuwa mtoto huyo hajanyanyaswa kingono.

Baadaye, mtoto huyo alirejeshwa katika hospitali ya CGTRH kwa uchunguzi zaidi ampapo fomu ya PRC ilijazwa na kuonyesha kuwa mtoto huyo hajanajisiwa.

Karatasi za mahakama zinaonyesha kwamba kuna mzozo kati ya mama ya mtoto huyo na familia ya baba mzazi kuhusu malezi yake.

Mahakama itatoa mwelekeo kuhusu kesi hiyo Desemba 13.

  • Tags

You can share this post!

Tumetokomeza kipindupindu, endeleeni na shughuli zenu,...

Hivi unazijua skendo za ‘Papa Mokonzi’ Koffi...

T L