• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Walevi, wamiliki baa Murang’a wampimia hewa Gavana Kang’ata

Walevi, wamiliki baa Murang’a wampimia hewa Gavana Kang’ata

NA MWANGI MUIRURI

MZOZO kati ya Gavana Irungu Kang’ata wa Murang’a na kamati ya kiusalama ya kaunti, umeendelea kutokotoa wakilaumiana ni nani anatepetea katika kutimiza ajenda ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kupunguza idadi ya baa.

Makundi haya mawili, yameonekana kulumbana kuhusu utoaji leseni za baa.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wamesema kwamba Kang’ata ameingiwa na hofu kuwa vita vya Gachagua dhidi ya baa huenda vikamsababishia uhasama miongoni mwa walevi na wamiliki wa baa hivyo basi kumponza kisiasa.

“Hizi sarakasi zote za Kang’ata ni hofu tu ya kisiasa. Katika mkutano wa Agosti 7, 2023 wa Rais Wiliam Ruto na magavana katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kang’ata na mwenzake wa Kiambu Kimani Wamatangi walizomewa sana na rais kuhusu leseni za baa na wakaambiwa warekebishe hali ili iwiane na sera ya kupunguza ulevi mashinani,” akasema mmoja wa maafisa wa Ikulu.

Afisa huyo aidha alisema kwamba Rais Ruto na Bw Gachagua tayari wametoa onyo kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2027, hawataunga mkono wanasiasa walio mamlakani kwa sasa na ambao hawataonyesha kujituma katika vita dhidi ya ulevi na mihadarati.

Wasiwasi huo ndio sasa unasemwa kuzindua sarakasi za Kang’ata kuwalaumu maafisa wa kiusalama, nao maafisa hao wakijibu kwa kujiondolea lawama lakini wakiwa na tabasamu kwa kuwa baadhi yao, inasemekana, huchukua mlungula kutoka kwa kila baa hivyo basi furaha yao ni baa zikiwa nyingi.

Mnamo Agosti 22, 2023 Kang’ata aliita kikao na waandishi wa habari na akatangaza kwamba maafisa wa kiusalama ndio wamezembea katika kutoa orodha ya wanaofaa kushiriki biashara ya uuzaji wa vileo ndani ya maduka maarufu kama Wines and Spirits.

“Sisi kama kaunti hatujatoa leseni hata moja ya maduka hayo. Tunagojea orodha ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya kutupa mwongozo wa ni nani anapaswa kuwa katika biashara hiyo,” akasema Kang’ata.

Kamishna wa Kaunti hiyo Bw Patrick Mukuria alijibu kwamba “hakuna wakati wowote sisi tulipewa wajibu wa kutoa leseni hizo wala ruhusa ya uendelezaji biashara hiyo kwa kuwa ni jukumu la serikali ya kaunti”.

Lakini Bw Kang’ata alisema ikiwa hakuna leseni yeye ametoa kwa maduka hayo, basi maafisa wa polisi ambao wamewajibishwa jukumu la utekelezaji sheria ndio wanapaswa kuchukulia hatua wanaokiuka sera hiyo.

“Mimi naomba maafisa wa kiusalama wawachukulie hatua wanaokaidi sheria katika biashara ya pombe,” akasema.

Hata hivyo, Kamanda wa polisi Murang’a Bw Mathiu Kainga alisema idara ya usalama inategemea serikali ya kaunti kufanikisha vita dhidi ya pombe haramu.

Alihoji, maafisa wa polisi wanakabiliwa na kibarua kigumu hasa wanapovamia baa inayouza pombe hatari na kupata ina leseni.

Bw Kainga alisema kwamba utekelezaji sheria unahitaji kila taasisi ya utawala itekeleze majukumu yake katika kuimarisha sera za serikali.

Huku mvutano huo ukiendelea, makundi ya kidini, kina mama na vijana yanazidi kushinikiza sera hiyo ya kupunguza baa itekelezwe mara moja.

Aidha, yanalia kutwikwa mzigo wa umasikini, mauti na magonjwa na jinamizi la ulevi na utumizi mihadarati.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Vikosi vya ujasusi, EACC kuwa macho usajili wa makurutu wa...

Mhadhiri atiliwa ‘mchele’, agundua kilabuni kuna walimu...

T L