• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wanahabari Nakuru wapanda miti kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 

Wanahabari Nakuru wapanda miti kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 

NA MERCY KOSKEI

WANAHABARI mjini Nakuru Jumatano waliungana kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa kupanda miti kwa minajili ya kutunza mazingira.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Chuo Kikuu cha Egerton, Njoro, zaidi ya wanahabari 50 kutoka mashirika mbalimbali walijitokeza kuhudhuria siku hii muhimu.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw Joseph Openda wa Shirika la NMG, walisema kuwa licha ya waandishi mara kwa mara kulalamika kuhusu haki zao bado wanapitia changamoto.

Bw Openda alisikitika kuwa baadhi ya waandishi na vyombo vya habari vinaendelea kukabiliwa na unyanyasaji na vitisho kutoka kwa serikali na mashirika mengine yanapoanikwa kwa ufisadi na maovu.


Wanahabari wa Nakuru wakipanda miti kuadhimisha siku ya vyombo vya habari duniani. Picha / Bonfance Mwangi

“Kwa muda mrefu wanahabari wamekuwa wakipitia changamoto ila tunaomba waweze kupatiwa uhuru wao wa kufanya kazi mahala popote muradi tu wanajuza umma yanayoendelea. Sherehe ya mwaka huu tulitaka iwe tofauti na ile ambayo tumezoea kuandamana barabarani; tuliamua tupande miti ili kuboresha mazingira,” alisema Openda

Bw Openda alsiema kuwa  waandishi wanapaswa kupata uungwaji mkono kutoka kwa mashirika ya kiserikali na washikadau wote ili kurahisisha kazi yao ya kupeperusha habari kwa umma.

Hata hivyo, alitoa wito kwa wanaomiliki vyombo vya habari kuwezesha wanahabari wao kwa kuwapa mafunzo mara kwa mara kwani ni muhimu

Mwanahabari huyo aidha alikashifu vikali mashambulizi dhidi ya wananahabari waliokuwa wakifuatilia maandamano ya muungano wa Azimio la Umoja awali jijini Nairobi, kadha wakijeruhiwa vibaya.


Wanahabari wa Nakuru wakipanda miti kuadhimisha siku ya vyombo vya habari duniani. Picha / Bonfance Mwangi

Kwa upande wake Mumbi Wambogo ripota wa K24, alisema kuwa wanasiasa wanaendelea kuchochea umma dhidi ya wanahabari hivyo basi kuwapa nyakati ngumu kusaka habari.

Akizungumza baada ya shughuli ya upanzi wa zaidi ya miche 500, Profesa Paul Kimurto, Mhadhiri Egerton alipongeza wanahabari kwa kujitolea kudumisha mazingira akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Bw Kimurto alisikitika kuwa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha majanga kama vile ukame, mafuriko, mifumo ya mvua isiyotabirika na  mlipuko wa magonjwa.

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa kujifanya ‘chokoraa’ akiuza chang’aa

Muuzaji nyama taabani kwa kuiba pesa za mauzo

T L