• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Ashtakiwa kwa kujifanya ‘chokoraa’ akiuza chang’aa

Ashtakiwa kwa kujifanya ‘chokoraa’ akiuza chang’aa

NA TITUS OMINDE

MCHUUZI maarufu wa pombe haramu kwenye kingo za mto Sossian katika mji wa Eldoret ambaye amekuwa akijifanya kuwa mmoja wa familia za kurandaranda mjini alishtakiwa katika mahakama ya Eldoret baada ya kupatikana na lita 395 za chang’aa.

Pamela Ong’ong’a alikamatwa na maafisa wa kudumisha sheria za Kaunti ya Uasin Gishu, kufuatia taarifa kutoka kwa wananchi katika eneo la Maangula kando ya mto Sossian, eneo ambalo ni maarufu kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bi Ong’ong’a ambaye alifika mbele ya Hakimu mkuu mkazi wa Eldoret Keyne Odhiambo alikanusha shtaka hilo.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Aprili 30, katika ukingo wa mto Sosian jini Eldoret alipatikana akiuza lita 395 za chang’aa ambazo alikuwa nazo bila leseni kinyume na kifungu cha 8(c) cha sheria ya vileo ya mwaka 2014.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200, 000 au mbadala wa pesa taslimu Sh70, 000.

Ajabu ni kwamba wateja wake walihamasishana kabla ya kuchanga dhamana ya Sh70, 000 pesa taslimu.

Kesi hiyo itatajwa Mei 15.

Kushtakiwa kwake kunajiri kufuatia msako mkali dhidi ya pombe haramu unaoongozwa na mwenyekiti wa bodi ya leseni na udhibiti wa vileo katika kaunti ya Uasin Gishu Koiya Maiyo.

Bw Maiyo alikuwa amefichua mapema kwamba maafisa wake wako macho kufuatia visa vilivyoripotiwa vya biashara haramu iliyokithiri kando ya mto Sosian.

Alisema kuna baadhi ya watu wanaojifanya jamii ya mtaani ambao wamegeuza maeneo ya kando ya mto kuwa mashimo ya kunywea pombe na maeneo ya kuuza dawa za kulevya.

Alitahadharisha familia za mitaani zinazojihusisha na biashara haramu kando ya mto huo.

  • Tags

You can share this post!

Baunsa taabani kwa kumjeruhi mteja klabuni

Wanahabari Nakuru wapanda miti kuadhimisha siku ya Uhuru...

T L