• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Wazee Lamu wataka serikali kuwachunguza wanasiasa wenye mienendo ya kutiliwa shaka

Wazee Lamu wataka serikali kuwachunguza wanasiasa wenye mienendo ya kutiliwa shaka

NA KALUME KAZUNGU

BARAZA la Wazee, kaunti ya Lamu sasa linaitaka serikali kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa ambao wamekuwa wakiingilia suala la usalama eneo hilo.

Kaunti ya Lamu imekuwa ikigonga vichwa vya habari kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Kati ya Juni na Septemba 2023, zaidi ya watu 30, ikiwemo walinda usalama na raia wameuawa ilhali nyumba zaidi ya 20 na kanisa zikiteketezwa moto na magaidi wa Al-Shabaab ambao mara nyingi wamekuwa wakitorokea msitu wa Boni.

Hayo yakijiri aidha, baadhi ya wanasiasa wa Lamu wamekuwa wakiendeleza malumbano majukwaani na hata kunyosheana kidole cha lawama kuhusiana na  mauaji ambayo yamekuwa yakiendelezwa na Al-Shabaab eneo hilo.

Wakizungumza na Taifa Leo Ijumaa, wanachama wa baraza hilo walisema suala la usalama si la kuingizwa siasa na kuhoji kwa nini baadhi ya viongozi wa kisiasa wa Lamu wamekuwa wakiendeleza matamshi yasiyofaa na hata kulaumiana kuhusiana na utata wa usalama.

Msemaji wa Baraza hilo, Mohamed Athman, aliwashauri wanasiasa kukoma kusimama majukwaani na kujadili suala la usalama alilolitaja kuwa nyeti.

Bw Athman alimpongeza Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithuire Kindiki kwa tangazo lake la hivi majuzi la kuwapiga marufuku wanasiasa wa Lamu kwenye vikao vyake vya kujadili suala la usalama.

Wakati wa ziara yake kisiwani Faza juma lililopita, Profesa Kindiki alieleza kusikitishwa kwake na hulka ya wanasiasa aliowataka kuwa ‘viherehere,’ ambapo wamekuwa wakiwalaumu walinda usalama na kuwakejeli kwamba wameshindwa kabisa kukabiliana na kumaliza magaidi Lamu.

“Mimi huudhika ninaposikia baadhi ya wanasiasa wakieneza matamshi potofu na yasiyo ya kizalendo eti wanawakemea walinda usalama wetu kwamba wamefeli kudhibiti usalama eneo hili. Huo mchezo ukome. Wiki hii tulipoteza watu mikononi mwa hawa magaidi, ikiwemo wanajeshi wetu. Ingekuwa maafisa wetu ni wazembe, itakuwaje wapatikane wakipambana na hawa wahalifu hadi wengine wao wapoteze maisha? Natakja niseme baadhi ya wanasiasa wa hapa tutakosana vibaya,” akasema Prof Kindiki.

Akaendelea, “kuanzia leo, mimi sitaki mwanasiasa yeyote katika mkutano wangu wa kuhusu usalama. Ukitaka kuchapa siasa zako, nenda mahali kwingine ukafanye hivyo na wala sio mikutano yangu. Mimi sitafuti kura, sitafuti kupendwa wala kuchukiwa bali natafuta kulinda wananchi, maisha na mali yao na kuhakikisha nchi yetu iko salama. Kwa hivyo mambo ya wanasiasa kuja kwa mikutano ya kiusalama na kisha kuleta visanga, sarakasi na kutusi maafisa wetu wa usalama ambao wengine wamelipa gharama ya juu zaidi ya kifo wakitulinda, mimi sitakubali.”

Bw Athman alisema mbali na Profesa Kindiki kuwapiga marufuku wanasiasa wa Lamu kuhudhuria mikutano ya kiusalama, ipo haja ya baadhi yao ambao wanaendelea kukaidi amri na kujadilia usalama kwenye majukwaa yao ya kisiasa wachunguzwe mara moja na kuadhibiwa.

Bw Athman alisema kama Baraza la Wazee wa Lamu, hivi karibuni watawaita viongozi wote wa kisiasa pamoja ili kutafuta mwafaka wa jinsi watakavyoheshimiana na kuepuka kujadili usalama majukwaani.

“Hata iwe kiongozi yeyote yule wa kisiasa ana cheo kikubwa namna gani, ni tajiri wa kiasi gani, ana ushawishi wa hali gani, lazima aheshimu idara ya usalama. Sisi kama wazee wa hapa kamwe haturidhiswi na hali inavyoendelea. Haiwezekani wanasiasa wetu kuingiza siasa kila jambo, ikiwemo hili nyeti la usalama. Lazima waepushe kabisa kujadilia usalama kwenye majukwaa yao ya kisiasa. Wakati pia umewadia kwa serikali kufuata kwa karibu mienendo ya wanasiasa wetu, wawakamate na kuwaadhibu wanaohusisha usalama na siasa,” akasema Bw Athman.

Kauli yake iliungwa mkono na mwenzake, Shee Mbwana aliyesisitiza haja ya wanaisasa wa Lamu kuiunganisha jamii na kuhubiri amani badala ya migawanyiko.

“Adui huja na propaganda ya chuki na kutugawanya. Hii ina maanisha lazima sisi nasi tutafute mbinu zitakazotuwezesha kuendeleza umoja na kupinga propaganda za magaidi. Viongozi wetu wa kisiasa ikiwa watatugawanya kwa matamshi yao ina maanisha adui ashinde na kuleta uharibifu zaidi. Tuchunge ndimi zetu,” akasema Bw Mbwana.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya mashakani Tanzania kwa kuishi nchini humo bila kibali

Wanaharakati washinikiza mkuu wa TSC Nancy Macharia ajiuzulu

T L