• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Amerika yakataa nguo kutoka Kenya biashara ya mitumba nayo ikitikiswa

Amerika yakataa nguo kutoka Kenya biashara ya mitumba nayo ikitikiswa

ANTHONY KITIMO Na MARY WANGARI

SERIKALI ya Amerika imepiga marufuku shehena ya nguo za watoto zilizoshonwa Kenya, kwa madai kuwa ni hatari kwa afya ya watoto.

Tume ya Usalama wa Bidhaa za Watumizi (CPSC) ilisema long’i hizo aina ya jeans zina vifungo vya vyuma ambavyo vinaweza kung’oka kwa urahisi na watoto kumeza kisha kunyongwa. Ilidaiwa kisa kimoja aina hiyo kilisharipotiwa Amerika.

Tume hiyo iliagiza zaidi ya long’i 100,000 za watoto ambazo zilikuwa zishafika katika maduka mbalimbali nchini humo, zisiuziwe wateja.

Tume hiyo ilitoa agizo hilo Agosti 10, na kutaka watu ambao walikuwa washanunua mavazi hayo wayarudishe katika maduka walikonunua na warudishiwe pesa zao.

Mavazi hayo yalikuwa yanauzwa Amerika na Canada tangu Septemba mwaka uliopita, kila vazi likiuzwa kwa Sh3,750.

Kenya hupeleka nguo hizo mpya Amerika chini ya makubaliano ya Sheria ya Nafasi ya Kukuza Afrika (AGOA) ambayo huwapa watengenezaji nguo wa mataifa ya Afrika kipaumbele kuingia kwa soko la Amerika.

Haya yanajiri huku serikali ikionekana kubadili msimamo wake kuhusu biashara ya mitumba huku ikipanga kutoza ushuru wa asilimia 25.

Ingawa biashara hiyo hufanywa na mahasla, ushuru anaopendekezwa Waziri wa Biashara Moses Kuria huenda ukasababisha wengi kufunga kazi zao.

Msimamo huu mpya ni kinyume na ahadi ya Kenya Kwanza ambayo viongozi wake walimkemea vikali kinara wa Azimio Raila Odinga alipodai mitumba ni mavazi ya maiti.

Waziri Kuria amependekeza mavazi yote yanayoingizwa nchini kutoka mataifa ya kigeni ikiwemo mitumba kuanza kutozwa ushuru wa asilimia 25, hatua anayosema inalenga kufufua sekta ya kilimo cha pamba.

Akizungumza Jumanne mjini Eldoret katika Kongamano la Ugatuzi, Waziri alisikitika kwamba sekta ya pamba nchini imewapa ajira watu wapatao 50,000 pekee badala ya mamilioni katika msururu wote wa kuongeza thamani.

“Kama taifa, tuna sekta yenye uwezo mkuu ya magora (vitambaa) lakini imesakamwa na bidhaa zinazoagiziwa kutoka nje. Kiwanda cha magora kinapaswa kupanuliwa ili kuwafaidi Wakenya na kwa madhumuni ya kuchochea ukuaji wa kiwanda hicho, tunahitaji kudhibiti magora yanayoingizwa nchini,” alisema Bw Kuria.

Aidha, alisema serikali itawasilisha mswada katika bajeti ya mwaka huu wa kutoza magora yanayoingizwa nchini kutoka nchi za kigeni ushuru wa asilimia 25 akihoji mavazi hayo yanapaswa kuchukuliwa kama bidhaa za kifahari.Alisema serikali itawezesha kuwepo mavazi ya bei nafuu ili kuhimiza wafanyabiashara kununua nguo zinazotengezwa humu nchini.

Kufuatia hatua hii, serikali ya Rais William Ruto imeonekana kubadili msimamo wake baada ya kumkashifu vikali Bw Odinga kwa kusema usimamizi wake utapatia kipaumbele mavazi yanayotengezewa humu nchini alipokuwa akigombea urais mwaka 2022.

“Watu wetu wanavalia tu nguo kutoka nje ya nchi ambayo tayari yamevaliwa na wafu,” alisema Bw Raila, kauli iliyoibua hisia mseto kote nchini.

“Ninasema hatumwondoi yeyote kwenye biashara. Tutahakikisha wanaoagizia mitumba kutoka mataifa ya kigeni wanapata fursa ya kwanza kutangaza bidhaa zinazoundwa kutoka humu nchini.”

  • Tags

You can share this post!

Wavuvi 200 walifariki kabla ya kuonja fidia ya Lapsset...

Huenda Mandago alichokoza nyuki kabla ya kukamatwa kwake,...

T L