• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Huenda Mandago alichokoza nyuki kabla ya kukamatwa kwake, kwa kushtaki Murkomen kwa Riggy G

Huenda Mandago alichokoza nyuki kabla ya kukamatwa kwake, kwa kushtaki Murkomen kwa Riggy G

NA SAMMY WAWERU

SENETA wa Kaunti ya Uasin Gishu, Jackson Mandago, alimsihi Naibu Rais Rigathi Gachagua kumshauri Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen jinsi serikali ya Kenya Kwanza inavyofanya kazi, kabla kisa cha Mpango wa Masomo wa Finland kumfika.

Wakati wa ziara ya Naibu Rais Gachagua mapema wiki hii katika sehemu mbalimbali Bonde la Ufa, Bw Mandago alisema kuwa Waziri Murkomen alihitaji kuelewa jinsi utawala wa Kenya Kwanza unahudumu.

Alirejelea kauli ya awali ya Naibu Rais, kwamba serikali ya Rais William Ruto ni sawa na kampuni ya hisa, hivyo basi wanaopaswa kunufaika ni walioiweka madarakani.

Gachagua alisema, “Utawala wa Kenya Kwanza unafanana na kampuni ya hisa, na wale wanaopaswa kupewa kipaumbele ni walioifanyia kampeni na kuichagua”.

Hata ingawa kauli ya Gachagua inafasiriwa kama kejeli za mishemishe za kisiasa, ilikosolewa pakubwa na upinzani – Azimio la Umoja.

Akizungumzia wakazi wa Eldoret wakati wa ziara ya Naibu Rais, Bw Mandago alimwomba Gachagua kuongea na Waziri Murkomen kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara Uasin Gishu.

Mandago aidha alilalamikia kwamba Waziri wa Barabara anaegemea maeneo mengine ya nchi na kusahau Uasin Gishu, akihoji kaunti hiyo ilichangia pakubwa kwa kapu la kura za Kenya Kwanza.

“Riggy G (jina la utani la Gachagua), ulitaja kwamba serikali hii inafanya kazi kama kampuni ya hisa. Barabara katika Kaunti ya Uasin Gishu pia inapaswa kupewa kipaumbele. Nimeona kujitolea kwa Waziri Kipchumba Murkomen kwa maendeleo ya nchi. Nilimwona Bondo. Anafanya kazi bora, lakini ni muhimu pia kumwelezea fomula ya Kenya Kwanza,” Mandago alisema.

Wakati akitoa kauli hiyo tata, Naibu Rais Gachagua alikuwa akikosoa Azimio la Umoja-One Kenya, akibainisha kwamba licha ya viongozi wa upinzani kuendelea kulaani serikali ya Kenya Kwanza, hawatakuwa na fursa ya kuwa sehemu yake.

Bw Gachagua alisisitiza kuwa ni wale tu waliokampeni na kupiga kura kwa ajili ya serikali ya sasa ndio watakaonufaika.

Mandago amejikuta mashakani kutokana na Mpango wa Masomo ya Finland na Canada, ambao umesababisha wazazi na wanafunzi kupoteza mamilioni ya pesa.

Mwaka 2021, akiwa Gavana wa Uasin Gishu, alizindua mradi huo ambao sasa imebainika ulikuwa wa viongozi wachache kujinufaisha.

Alikamatwa Jumatano, Agosti 16, 2023 na kuachiliwa na mahakama kwa dhamana mnamo Alhamisi.

 

  • Tags

You can share this post!

Amerika yakataa nguo kutoka Kenya biashara ya mitumba nayo...

Azimio wamponda balozi wa Amerika

T L