• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Bei ya maji Nairobi na Mombasa kupanda

Bei ya maji Nairobi na Mombasa kupanda

NA CHARLES WASONGA

HUENDA bei ya maji ikapanda katika kaunti za Nairobi, Mombasa na nyingine zisizosalisha maji yao ikiwa mswada uliowasilishwa juzi bungene utapitishwa kuwa sheria.

Mswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Maji ya 2023 uliowasilishwa bungeni na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa, unapendekeza kuwa Nairobi na kaunti nyingine ambazo zinategemea maji kutoka kaunti nyinginezo, zinunue rasilimali hiyo kutoka kwa mashirika ya maji yanayosimamiwa na serikali kuu.

Kulingana na mswada huo, Kaunti ya Nairobi, kwa mfano, italazimika kununua maji kutoka kwa Shirika la Athi Water Development Agency.

“Mswada huu unapendekeza kuifanyia mabadiliko sehemu ya 100 ya sheria hiyo ili kutoa nafasi kwa usambazaji wa maji kwa wingi katika kaunti na mashirika ya maji yaliyoundwa kwa mujibu wa sheria hii,” unasema mswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo Alhamisi Julai 6, 2023.

Hii ndiyo siku ambayo Bunge la Kitaifa liliahirisha vikao vyake kutoa nafasi ya mapumziko ya wiki mbili kwa wabunge.

Mswada huo umewasilishwa bungeni wiki mbili baada ya Waziri wa Maji na Unyunyiziaji Alice Wahome kufichua kuwa serikali inapanga kuilipisha Nairobi kwa maji inayotumia. Alisema pesa ambazo Nairobi italipa zitatumika kugharimia ustawishaji wa chemchemi za maji na miundomsingi.

“Tunaandaa sheria na ikipitishwa, serikali kuu itatia mkataba na Nairobi kuhusu ununuzi wa maji kwa wingi. Hatua hii italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya maji,” akasema Bi Wahome.

“Hizi ndizo pesa tutakazozitumia kustawisha vianzo vya maji na vifaa muhimu,” akaongeza.

Wakati huu Nairobi hailipa kaunti husika au serikali kuu kwa maji inayopata na kuuza kwa wakazi kupitia Kampuni ya Maji na Maji-taka ya Nairobi (NCWSC).

Kaunti ya Nairobi hupata maji kutoka kwa mabwawa ya Ndakaini, Sasumaa, Konoike na Bwawa la Thika.

Bwawa la Ndakaini liko kaunti ya Murang’a, mabwawa ya Konoike na Sasumaa yanapatikana Nyandarua huku bwawa la Thika likiwa rasilimali ya kaunti ya Kiambu.

Sheria hiyo inalenga kuzifanya kaunti zisizosalisha maji yao kuwajibika zaidi na kukoma kuweka mikakati ya kutunza rasilimali hiyo kwa kuzuia wizi na uharibifu wa mabomba ya maji.

Kaunti nyingine ambayo itaathiriwa na sheria hii ni Mombasa ambayo hupata maji yake kutoka kaunti jirani za Kwale, Kilifi na Taita Taveta. Vianzo vya maji hayo ni visima vya Tiwi (Kwale), Baricho (Kilifi) na Mzima (kaunti ya Taita Taveta).

  • Tags

You can share this post!

DCI Murang’a: Ako wapi Esther Ruguru aliyetoweka...

Hatupangi ‘mapinduzi’ kwa kukusanya saini...

T L