• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Hatupangi ‘mapinduzi’ kwa kukusanya saini – Karua

Hatupangi ‘mapinduzi’ kwa kukusanya saini – Karua

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Narc Kenya Martha Karua amefafanua kuwa mchakato ulioanzishwa na Azimio La Umoja-One Kenya wa kukusanya saini unalenga tu kupata idadi ya watu wasioridhika na serikali ya Kenya Kwanza na wanaounga mkono kampeni zao.

Akihojiwa katika kituo cha redio cha Spice FM, Bi Karua alionekana kukwepa dhana ya wengi kwamba lengo la ukusanyaji wa saini hizo zisizopungua 10 milioni ni kumwondoa mamlakani Rais William Ruto.

“Saini hizo zitatusaidia kujua idadi ya watu wanaounga mkopo kampeni zetu za kupinga mapendekezo dhalimu kwenye Sheria ya Fedha ya 2023 na sera nyingine mbovu za utawala wa Kenya Kwanza. Saini hizo pia zinalenga kutoa hesabu ya Wakenya ambao wameamua kutekeleza mamlaka yao moja kwa moja,” Bi Karua akasema huku akiongeza kuwa malalamishi ya Azimio yanafanana na yale ya Wakenya.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alizindua mchakato huo wa ukusanyaji sahihi mnamo Ijumaa Julai 7, 2023 katika mkutano wa Saba Saba iliyoandaliwa katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi.

“Mamlaka ni ya wananchi na hicho ndicho kipengee cha kwanza cha Katiba,” akasema.

“Na wananchi wako na uwezo wa kumpokonya kiongozi yeyote mamlaka hayo. Hii ndio maana leo (Ijumaa) tutaanzisha shughuli za ukusanyaji wa saini,” Bw Odinga akasema.

Kauli ya Bi Karua inaonekana kufanana na ile aliyotoa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka mnapo Jumapili ambaye alisema kuwa “lengo la Azimio sio kumpokonya mtu yeyote mamlaka bali ni kuonyesha kuwa wananchi ndio wenye mamlaka makuu nchini wala sio viongozi”.

“Msiwe na wasiwasi. Saini ambazo tutakusanya ni za wale Wakenya wanaolalamikia kupanda kwa gharama ya maisha kutokana na kupandishwa kwa ushuru,” akasema Bw Musyoka alipowahutubia wanahabari baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika eneo la Kathiani, Kaunti ya Machakos.

  • Tags

You can share this post!

Bei ya maji Nairobi na Mombasa kupanda

Omanyala na wenzake mawindoni kutafuta tiketi ya riadha za...

T L