• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Bewa la MKU Rwanda sasa ni Mount Kigali University

Bewa la MKU Rwanda sasa ni Mount Kigali University

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ya Rwanda imetoa kibali maalum kwa bewa la Chuo Kikuu cha Mount Kenya nchini humo na kulipandisha hadhi liwe chuo kikuu kinachojitegemea kwa jina Mount Kigali University of Rwanda.

Kulingana na ujumbe maalum kutoka kwa serikali ya Rwanda mpango huo umekamilika rasmi.

Mpango huo ulipitishwa katika mkutano wa baraza la mawaziri uliongozwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame mnamo Aprili 20, 2023.

Naibu Chansela wa chuo hicho nchini Rwanda, Profesa  Edwin Odhuno, aliyekuwepo kabla ya mabadiliko hayo, alipongeza serikali hiyo kwa hatua ilizochukua.

“Tunapongeza Wizara ya Elimu ya Rwanda kwa kuleta mabadiliko hayo. Hata tulipopata ujumbe huo wanafunzi wengi walifurahia hatua hiyo muhimu,” alisema Prof Odhuno.

Alisema kibali hicho cha kulifanya bewa hilo kuwa chuo kamili nchini Rwanda kinafanya iwe rahisi kufanya utafiti na kufikia umma hasa maeneo ya mashinani.

Kwa wakati huu chuo hicho kina wanafunzi wapatao 6,000 ambao wanatarajiwa kujikakamua na kuonyesha ubora wao wakiwa hapo.

Prof Odhuno alisema ana imani ya kwamba mwenyekiti na mwanzilishi wa MKU Profesa Simon Gicharu, atakuwa mstari wa mbele kukisaidia chuo kikuu hicho kupanda hadhi ya juu zaidi.

“Tumekuwa tukiendesha chuo hiki kwa zaidi ya miaka 13 kupitia uboreshaji wa miundomsingi, vifaa muhimu vya masomo na tunatarajia kupiga hatua za juu zaidi,” alisema Prof Odhuno.

Mwanafunzi Damalie Tumushime amepongeza nchi yao kwa kujizatiti kuwa na chuo kikuu kinachotambulika nje ya nchi.

“Sasa hatutakuwa na wakati ngumu wa kusafiri hadi Chuo Kikuu cha Mount Kenya huko Thika ili kufuzu kama walivyokuwa wakifanya wanafunzi waliotutangulia hapa. Lakini tutapata nafasi ya kukamilisha masomo yetu hapa nchini,” alisema Bw Tumushime ambaye ni mwanafunzi katika chuo hicho kipya cha Rwanda.

Naye Ronald Nkuso ambaye pia ni mwanafunzi hapo alisema watapata kazi rahisi ya kukamilisha masomo yao hapo chuo bila kusafiri hadi MKU mjini Thika nchini Kenya.

Hapo awali chuo hicho kilizindua kitabu maalum cha ‘Mountain Meets Land Of 1,000 Hills’.

Kitabu hicho kiliangazia maswala mengi kuhusu nchi ya Rwanda na mienendo ya kimaisha huko.

Walibuni pia wakfu wa Imbuto kuangazia watoto wa kike na kuwapa sapoti wafaulu maisha yao ya baadaye. Wakati wa uzinduzi huo, Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichangisha kiwango cha RWF 36,750,000 sawa na Sh4.5 milioni, huku wakiweka mkataba wa miaka mitano.

  • Tags

You can share this post!

DKT FLO: Nakerwa na hali ya mchumba wangu kukoroma anapolala

Magavana watishia kugoma

T L