• Nairobi
  • Last Updated June 14th, 2024 2:05 PM
Brian Mwenda anayedaiwa kuwa ‘wakili feki’ ashtakiwa Milimani

Brian Mwenda anayedaiwa kuwa ‘wakili feki’ ashtakiwa Milimani

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) amemfikisha kortini Brian Mwenda Njagi kwa madai alijifanya wakili.

Mwenda anayedaiwa alighushi cheti cha Chama cha Wanasheria Nchini (LSK), alifikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Mahakama ya Milimani Bw Lucas Onyina akikabiliwa na mashtaka sita ya ulaghai.

Shtaka lilisema kati ya Agosti 30, 2022, na Machi 3, 2023, Mwenda alijitengenezea cheti cha kujiunga na LSK kikiwa na nambari p.105/201249/22 kwa jina la Brian Mwenda N.

Hakimu alifahamishwa Mwenda alijifanya cheti hicho kilikuwa halisi kilichotayarishwa na LSK na kwamba angehudumu kama wakili katika Mahakama Kuu.

Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka kwamba Mwenda alijifanya cheti hicho alichoghusi kilikuwa kimetolewa na Msajili wa Mahakama Kuu Bi Anne Amadi.

Shtaka la pili lilikuwa kwamba Mwenda alimkabidhi Wakili Mwangi Kiai cheti hicho katika afisi yake eneo la Westlands jijini Nairobi.

Mwenda alishtakiwa kujizolea cheti cha kuhudumu cha mwaka wa 2023 akidai cheti cha uwakili nambari p.105/201249/22 kilikuwa halisi.

Mnamo Oktoba 9, 2023, katika  afisi ya mawakili ya Micheka Omwenga & Co. Advocates akiwa na nia ya kudanganya, alitoa cheti chake cha uwakili nambari p.105/201249/22 akidai kilikuwa halisi na kwamba kimeidhinishwa na Msajili wa Idara ya Mahakama Kuu.

Mwenda alishtakiwa kumdanganya wakili Bw Kiai mnamo Machi 3, 2023, kwamba alikuwa amehitimu kuwa wakili.

Shtaka la sita dhidi ya Mwenda lilikuwa la kuiba kitambulisho cha LSK mnamo Agosti 14, 2023, kilichokuwa kimetolewa rasmi kwa wakili Brian Mwenda Ntwiga (ambaye ni wakili wa serikali katika afisi ya Mwanasheria Mkuu).

Mwenda aliyelipiwa dhamana ya polisi mnamo Oktoba 17, 2023, na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, alikanusha mashtaka hayo.

Mawakili Dkt John Khaminwa na Danstan Omari waliomwakilisha walipinga Rais wa LSK Erick Theuri akishiriki katika kesi kwa niaba ya LSK wakisema “atakuwa shahidi.”

Bw Omari alisema pia kiongozi wa mashtaka Bw J V Owiti pia hastahili kuongoza kesi hiyo kwa vile pia atakuwa shahidi katika kesi hiyo.

Lakini Dkt Khaminwa alilumbana na Bw Owiti alipopinga akiomba mahakama imzuie kushiriki katika kesi hiyo.

Dkt Khaminwa alisema kumshtaki Mwenda ni kuharibu wakati na rasilimali za serikali.

Lakini Mbw Theuri na Owiti walisema hawawezi kuzuiliwa kushiriki katika kesi hiyo kwa vile “haiwezekani mtu asiye wakili kujifanya wakili na kuendelea kuwatetea watu mahakamani kwa njia ya ujanja na udanganyifu.”

Bw Onyina atatoa uamuzi Alhamisi ikiwa LSK na Owiti watashiriki katika kesi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume aliniomba penzi, kabla sijamjibu asharukia na...

Jinsi mwasisi wa Mungiki alivyojiondoa kwa maisha ya kuua...

T L