• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
DPP apewa siku 14 kuandaa ushahidi katika kesi ya ‘wakili feki’

DPP apewa siku 14 kuandaa ushahidi katika kesi ya ‘wakili feki’

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amepewa siku 14 kukamilisha uchunguzi katika kesi ambapo Brian Mwenda ameshtakiwa kwa kujifanya wakili.

Agizo hilo lilitolewa Jumanne na hakimu mkuu katika Mahakama ya Milimani Lucas Onyina kufuatia ufichuzi kwamba polisi wanawasaka mashahidi kutoka asasi tano za serikali kurekodi ushahidi.

Akiwasilisha ombi kesi hiyo iahirishwe kwa siku 14, kiongozi wa mashtaka Bw Festus Njue alisema “ushahidi uliopo hautoshi kwa vile polisi wanaendelea na uchunguzi.”

Akasema Bw Njue: “Naomba kesi hii iahirishwe kwa siku 14 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi na kurekodi ushahidi kutoka kwa asasi tano za serikali.”

Bw Njue aliongeza kueleza mahakama kuwa ombi lake lisichukuliwe kana kwamba “DPP hana ushahidi.”

Hakimu aliombwa amkubalie DPP kusaka ushahidi ndipo kesi hiyo itengewe siku ya kusikilizwa.

Lakini wakili Danstan Omari alipinga ombi hilo na kuomba hakimu amwachilie huru Mwenda akisema DPP ameungama kortini hana ushahidi.

“Hatujakabidhiwa nakala za ushahidi na DPP. Ukweli ni kwamba DPP hana ushahidi. Kesi hii iliwasilishwa kwa sababu za siasa za Chama cha Mawakili nchini (LSK). Siku ile Mwenda alishtakiwa mahakama hii ilifurika mawakili na baraza kuu la LSK. Sasa mawakili hao wametoweka,” Bw Omari alimwelea hakimu.

Akinukuu Kifungu nambari 50 cha Katiba, Bw Omari alisema kila mshukiwa anafaa kupata haki mahakamani kwa kukabidhiwa nakala za mashahidi ajiandae namna ya kujitetea.

“Naomba umwachilie Mwenda kwa vile hakuna ushahidi. Ni siasa tu zilizofanya afikishwe kortini. Uchaguzi wa mwakilishi wa LSK katika Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama ni Februari 2024,” Bw Omari alidokeza.

Aliomba mahakama itengee kesi hii muda isikilizwe na kuamuliwa kabla ya Februari 2024.

Bw Onyina aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, 2023.

Mwenda amekana alijifanya wakili na kujipatia cheti cha uanachama wa LSK akidai kimeidhinishwa na  Msajili wa Idara ya Mahakama Bi Anne Amadi.

  • Tags

You can share this post!

Mabunge ya Kenya, Zambia yapigia debe chama chao cha...

Brown Mauzo na Vera Sidika kukutana uso kwa macho baada ya...

T L