• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Mabunge ya Kenya, Zambia yapigia debe chama chao cha Jumuiya ya Madola

Mabunge ya Kenya, Zambia yapigia debe chama chao cha Jumuiya ya Madola

NA BENSON MATHEKA

MABUNGE mawili ya nchi za Afrika, Zambia na Kenya, yameomba mabunge barani kutambua Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), kinacholeta pamoja mabunge katika nchi zinazostawi.

Juhudi za mabunge ya Kenya na Zambia zinajiri wiki chache baada ya kongamano la CPA ambalo lilifanyika Ghana mnamo Oktoba.

Shinikizo za “kutambuliwa ipasavyo” kwa CPA zilizidi baada ya Kamati za Biashara za Bunge ya nchi hizo mbili kukutana nchini Zambia.

Ujumbe wa Kenya unaongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, ambaye pia alikutana na mwenzake wa Zambia Nelly B.K. Muti.

Kamati hizo mbili zilibainisha kuwa kutambua CPA kutasaidia kuendeleza mchakato wa kutunga sheria barani Afrika.

Huku zikisisitiza juu ya umuhimu wa utambuzi unaohitajika sana, timu hizo mbili zilisema hii itasaidia katika uanzishaji wa mfumo wa kisheria ulioainishwa vyema na hivyo kuifanya kuwa ya manufaa kwa nchi wanachama.

Pia zilisema kuwa kutambuliwa kutahakikisha kwamba makoloni ya zamani ya Uingereza yatawakilishwa ipasavyo ndani ya Jumuiya ya Madola.

Mkutano huu wa hadhi ya juu pia ulitoa jukwaa mwafaka la kubadilishana mawazo kuhusu taratibu za bunge za mataifa yote mawili.

Washiriki walibadilishana maarifa muhimu katika muundo wa vyumba vyao vya kutunga sheria na kamati mbalimbali.

Mkutano wa Maspika hao wawili Wetang’ula na Mutti pia uliangazia uhusiano thabiti wa kiuchumi kati ya Zambia na Kenya, ukiwa na msisitizo maalum juu ya athari chanya ya wawekezaji wa Kenya wanaoendesha shughuli zao nchini Zambia.

Bw Wetang’ula alitumia fursa hiyo kumwalika Muti kuhudhuria maombi ya kitaifa mwaka ujao ambayo hufanyika kabla ya sherehe za Siku ya Madaraka.

Harakati za kutaka kutambuliwa na mkoloni wa zamani zinakuja wakati ambapo Kenya iko katika harakati za kuanzisha Kituo cha Mafunzo ya Bunge (CPST) kitakachotumika kama nyenzo ya kuwafunza wafanyikazi na wajumbe wanaohudumu katika mabunge kote Afrika na kuna uwezekano kitawanufaisha watu wa Zambia.

Wakati wa kikao hicho, Kamati ya Biashara ya Bunge la Zambia ilipongeza ufanisi wa Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge ya Kenya (CDF).

Hapo awali, Bw Wetang’ula alikutana na kutangamana na Wakenya wanaoishi Zambia kutafuta fursa za ushirikiano na nchi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Sarakasi Gavana Mwangaza akijadiliwa katika bunge la Seneti

DPP apewa siku 14 kuandaa ushahidi katika kesi ya...

T L