• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Duale afika Lamu kuziba vichochoro vya Al-Shabaab

Duale afika Lamu kuziba vichochoro vya Al-Shabaab

NA KALUME KAZUNGU

WAZIRI wa Ulinzi Aden Duale amewaonya wakazi wanaoshirikiana na magaidi wa Al-Shabaab ambao siku za hivi karibuni wamekuwa wakiwaua wananchi na walinda usalama, kaunti ya Lamu kwamba siku zao zimehesabiwa.

Akizungumza Jumamosi wakati wa ziara ya kutathmini hali ya usalama kaunti ya Lamu, waziri Duale aliweka wazi kuwa magaidi ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulio eneo hilo wanasaidiwa na baadhi yua wenyeji ambao huwapa chakula, mahali pa kujificha na pia kuwaelekeza kwa vijiji kuendeleza mauaji na uharibifu wa mali.

Kati ya Juni na Agosti mwaka huu, jumla ya watu 10, akiwemo mke wa diwani wa Hindi, James Njaaga, waliuawa ilhali nyumba zipatazo 20 zikiteketezwa kwa moto na magaidi waliovamia vijiji vya Juhudi, Salama, Widho, Marafa na viungani mwake.

Hali hiyo ilipelekea zaidi hya familia 400 kuishi kwenye kambi ya wakimbizi wa shule ya msingi ya Juhudi, Lamu Magharibi hadi sasa kwa kuhofia kulengwa na kuuawa na magaidi hao.

Bw Duale alisema serikali haitaendelea kukaa chini ikitazama wahalifu wakiendelea kuwahangaisha wananchi wasio na hatia.

Alisema hivi karibuni ofisi yake, kwa ushirikiano na ile ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Profesa Kithure Kindiki zitaorodhesha kwenye gazeti rasmi la serikali maeneo ya Lamu ambayo yatakuwa ni marufuku kwa makazi ya binadamu.

Maeneo hayo ni Tabasamu, Mkunumbi, Marafa, Ukumbi, Marafa Toto, Juhudi, Salama, Widho, Poromoko, Jirma na Pandanguo.

Maeneo hayo yanapatikana karibu na msitu wa Boni ilhali mengine yakiwa ndani yam situ huo mkubwa.

Bw Duale alisema watapasua barabara-mpaka ndani ya msitu wa Boni, ambapo watatangaza rasmi ni wapi wananchi wataruhusiwa kuishi ilhali sehemu nyingine iachiwe walinda usalama, hasa Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF) kuendeleza operesheni ya kukabiliana na kuangamiza maadui-Al-Shabaab.

“Mimi Waziri wa Ulinzi na mwenzangu Profesa Kithure Kindiki wa Usalama wa Ndani, tumeafikiana kupasua mpaka rasmi kwenye maeneo tuliyotaja. Tutatangaza kwamba mwananchi yeyote akionekana kwa hiyo sehemu ya barabara ambayo ni marufuku, iwe anaingia au kutoka ajue katu hatutamtambua yeye kama Mkenya. Tutakuchukulia wewe kuwa Al-Shabaab na tutapambana nawe vilivyo,” akasema Bw Duale.

Akitaja barabara sita za kaunti ya Lamu zitakazotengenezwa kupitia mwongozo wa KDF, Bw Duale aliwasihi wananchi kushirikiana vilivyo na vitengo vya usalama kumaliza kero la Al-Shabaab si Lamu pekee bali nchi nzima kwa ujumla.

Barabara hizo za usalama zitakazojengwa na KDF ni pamoja na ile ya kilomita 21 ya Witu-Pandanguo, barabara ya kilomita 40 ya Mkokoni-Kiunga, Bodhei-Kiunga, Pangani-Bodhei-Kiunga, Kiangwe-Basuba na Witu-Sendemke-Katsaka Kairu.

Waziri huyo aliwaonya wanasiasa wa Lamu dhidi ya kuingiza siasa suala la usalama.

“Wale wanaowaficha magaidi tunawajua na tutaanza kuwakamata. Ninaloomba ni wanasiasa, si gavana, seneta, mbunge, nyote muacha kunipigia simu endapo utapata fulani ametiwa mbaroni ili nimwachilie. Nyinyi mlipigiwa kura na kuingia uongozini, hivyo haina haja kuingilia kati kurai idara ya usalama kuwaachilia waliokamatwa kwani hatutakubali kamwe,” akasema Bw Duale.

 Waziri huyo hata hivyo aliwashukuru maafisa wake wanaotekeleza operesheni ya kiusalama msituni Boni na Lamu kwa ujumla kwa kuzuia maafa zaidi na mashambulio ya Al-Shabaab kila mara.

Aliahidi kuhakikisha kambi ya walinda usalama inabuniwa kwenye vijiji vya Lamu ambavyo kila mara vimekuwa vikishambuliwa na magaidi, hasa eneo la Juhudi ambako zaidi ya familia 400 zimepiga kambi kwa kuhofia usalama wao vijijini.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa Lamu. Amewaonya wanaowaficha Al-Shabaab kwamba zao zimehesabiwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wananchi waliohudhuria kikao walifurahia ziara ya Bw Kindiki, wakiitaja kujiri kwa wakatio ufaao.

“Niko na imani ziara ya Waziri Duale italeta suluhu ya kudumu katika kukomesha hayo mashambulio na mauaji tunayoshuhudia kila kuchao,” akasema Bi Pamela Ogutu.

Wakati wa ziara ya Jumamosi Lamu, Waziri Duale aliandamana na maafisa wa ngazi za juu wa KDF, akiwemo Meja-Jenerali, Juma Mwinyikai na Katibu wa Kudumu wa Uwekezaji, Abubakar Hassan.

Viongozi wa Lamu waliokutana na Bw Duale wakati wa ziara ya Jumamosi ni Gavana wa Lamu Issa Timamy, Mbunge wa Lamu Magharibi Stanley Muthama, yule wa Lamu Mashariki Kapteni Ruweida Obbo, Seneta wa Lamu Joseph Githuku Kamau, madiwani wa Lamu na wengineo.

Bw Duale alizuru Mokowe, Lamu Magharibi na Faza, Lamu Mashariki kabla ya kuhitimisha ziara yake.

  • Tags

You can share this post!

Ababu ataka wabaya wa Azziad wakome kuzua madai ya uongo...

Seneti kujadili hoja ya kuhalalisha Kamati ya Kitaifa ya...

T L