• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
El-Nino yalemea Pwani maafa yakishuhudiwa

El-Nino yalemea Pwani maafa yakishuhudiwa

KALUME KAZUNGU, JURGEN NAMBEKA NA CECE SIAGO

SEHEMU mbalimbali katika ukanda wa Pwani zimeathiriwa na mvua ya El-Nino inayoendelea kushuhudiwa katika sehemu tofauti nchini.

Katika kaunti ya Mombasa, maeneo ya Bamburi, Utange, Kiembeni wakazi walipatwa na taabu baada ya mafuriko kuwazuia hata kutoka nyumbani kwao.

Maelfu ya wakazi walisambaza picha mitandaoni kuelezea gadhabu yao kuhusu mvua hiyo iliyoanika mfumo duni wa usambazaji majitaka Kaunti ya Mombasa.

Katika eneo la Bangladesh, msichana wa Kidato cha nne aliaga dunia baada ya kukanyaga waya wa umeme uliokuwa majini.

Kulingana na afisa wa elimu wa kaunti ndogo ya Jomvu Bi Maimuna Ahmed, mwendazake alikuwa amekamilisha mtihani wake wa mwisho wa sekondari(KCSE).

Kwenye eneo la Majajani Kaunti ya Kilifi, mzee mmoja aliaga dunia baada ya kuporomokewa na nyumba.

“Tulimwomba Bw Kenga Baya aende akalale kwa wajukuu pamoja na familia yake ila akakataa kuwa hawezi kulala kwa wajukuu zake. Jamaa zake walikubali wito ila yeye aliyebaki tuliamkia habari za kuwa nyumba ilikuwa imeporomoka,” akasema jamaa yake Bw Sammy Kashindo.

Katika Kaunti ya Lamu, karibu wakazi 3,000 wa vijiji vya Pandanguo na Jima, tarafa ya Witu, walibaki katika hofu ya ukosefu wa chakula baada ya barabara yao ya pekee ya Pandanguo kuelekea Witu kukatika katika eneo la Ziwa la Kiboko.

Hii ni baada ya mafuriko yaliyochangiwa na mvua kubwa, inayoendelea kunyesha eneo hilo kwa karibu juma zima sasa.

Ikumbukwe kuwa barabara hiyo ndiyo kiunzi cha pekee kwa wakazi wa Pandanguo na Jima kufikia maduka na bidhaa yapatikanayo mji wa Witu.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali kwa njia ya simu, Mzee wa Nyumba Kumi katika kijiji cha Pandanguo, Bw Ali Sharuti alisema familia nyingi zimekuwa zikitatizika kupata chakula, ikizingatiwa kuwa eneo la kipekee kujinunulia bidhaa ni mji Wa Witu.

Bw Sharuti aliiomba serikali ya kaunti kushirikiana na ile ya kitaifa na mashirika, ikiwemo lile la Msalaba Mwekundu, kuwafikishia misaada ya chakula na vyandarua.

“Barabara yetu imekatika kumaanisha hatuwezi kufikia maduka kujinunulia chakula. Tunaomba hata kama ni ndege kupitia ufadhili wa kaunti, serikali kuu na mashirika itufikishie vyakula vya msaada, vyandarua na dawa za maji. Tunahofia baa la njaa na mlipuko wa maradhi vijijini mwetu,” akasema Bw Sharuti.

Kule Kwale, usafiri katika barabara kuu ya Likoni kuelekea Lungalunga ulikwama kwa siku ya pili huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha Kaunti ya Kwale na kusababisha mafuriko.

Mabasi, matrela na mamia ya abiria walilazimika kukesha usiku karibu na Daraja la Ramisi baada ya mto huo kuvunja kingo zake na kufanya barabara kutopitika.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Michael Meru, mvua kubwa inayoendelea kunyesha kwa siku ya tatu sasa, imesababisha mito yote katika kaunti hiyo kufurika.

Mito hiyo ni Ramisi, Mkurumudzi, Umbea, Mwena na Mbadi, huku akitoa onyo kwa wakazi wanaoishi sehemu za chini kuchukua tahadhari.

Katika eneo la Kinango, abiria waliokuwa kwenye gari la kibinafsi walinusurika kifo wakati gari lao lilisombwa na mafuriko walipokuwa wakijaribu kuvuka daraja lililofurika la Mto Mbadi.

Barabara ya Kinango kuelekea Kwale pia iliathirika magari yakikwama kwenye matope.

Hali ilikuwa iyo hiyo katika Kaunti ya Tana River.

 

  • Tags

You can share this post!

Familia yaomba msaada kurejesha maiti ya jamaa yao hapa...

Mswada wa kamari kulinda washindi kampuni zisiwapunje

T L