• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
EPRA yafeli kutoa afueni kwa Wakenya

EPRA yafeli kutoa afueni kwa Wakenya

NA CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Petroli (EPRA) imepunguza bei ya mafuta aina ya petroli kwa senti 0.85 kwa lita huku ikipunguza bei ya mafuta taa kwa Sh3.96.

Hata hivyo, kwenye bei mpya iliyoitangaza Julai 14, 2023 usiku, EPRA haijafanya mabadiliko yoyote kwa bei ya dizeli.

Hii ina maana petroli sasa itauzwa kwa Sh194.68 kwa lita jijini Nairobi kutoka bei ya Sh195.53 iliyowekwa Juni 30, 2023. Hii ni baada ya EPRA kukaidi agizo la mahakama na kuongeza ushuru wa VAT kwa bidhaa za petroli kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16.

Na bei dizei itasalia kuwa Sh179.69 kwa lita jijini Nairobi huku bei ya mafuta taa ikishuka hadi 169.48 kwa lita jijini Nairobi kutoka Sh173.44 iliyoanza kutumika Juni 30, 2023 usiku.

“Hizi bei mpya za bidhaa za petroli zitatumika kwa muda wa mwezi mmoja hadi Agosti 14, 2023,” ikasema taarifa kutoka EPRA iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu Daniel Kiptoo.

Mnamo Juni 30, 2023, EPRA iliongeza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa Sh13.49, Sh12.39 na Sh11.96 mtawalia iliyoanza kutumika kuanzia Julai 1, 2023.

Hii ni licha ya agizo la Mahakama Kuu lililotolewa na JajI Mugure Thande kuzuia serikali kutekeleza Sheria ya Fedha ya 2023, iliyoongeza VAT kwa bidhaa za petroli maradufu.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya 2013, ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya taa umeongezwa kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16 kuanzia Julai 1, 2023. Kufuatia mabadiliko hayo bei inayoruhusiwa za Petroli, Dizeli na Mafuta jijini Nairobi zimepanda kwa Sh13.49 kwa kila, Sh12.39 kwa lita na Sh11.96 kwa lita, mtawalia,” Kiptoo akasema.

Mnamo Jumatatu Julai 10, 2023, Jaji Thande alikataa kuruhusu utekelezaji wa Sheria ya Fedha, 2023 akisema kesi hiyo iliyowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtata “inayo masuala mazito ya kikatiba”.

Kwa hivyo, aliwasilisha faili ya kesi hiyo kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili abuni jopo la majaji watatu kuisikiliza na kutoa uamuzi.

Kufikia sasa, Jaji Koome hajabuni jopo hilo.

  • Tags

You can share this post!

NMG yapiga jeki Mbogolo ECD kwa msaada wa vitabu

Wafugaji waliovamia msitu wa Mukogodo kufurushwa

T L