• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Gachagua ‘aingizwa darasani’ baada ya kusema ana bidii ya fisi

Gachagua ‘aingizwa darasani’ baada ya kusema ana bidii ya fisi

NA LABAAN SHABAAN

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amegeuka gumzo mitandaoni baada ya kusema yeye ni mchapakazi kama fisi katika mahojiano na kituo cha redio kinachopeperusha matangazo kwa lugha ya Gikuyu cha Inooro FM.

Akitoa wito kwa viongozi na wakazi wa kutoka Mlima Kenya kuungana, Bw Gachagua alijipiga kifua kuwa yeye ana bidii kama fisi akitaka wengine serikalini kumuiga.

Lakini badala ya kuchukuliwa alivyopendelea, watumiaji wa mitandao ya kijamii wameonekana kutokubaliana na tashbihi aliyotumia kudhihirisha jitihada.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Rais aliwasihi watumishi wa umma wawe vielelezo na wafanye kazi kwa bidii.

“Ninaomba sisi sote katika serikali hii tufanye kazi kwa bidii. Tujiimarishe na tusijiaibishe kama jamii. Mimi ni kiongozi mfano bora. Ninafanya kazi kama fisi. Viongozi wote wa Mlima Kenya wanaofanya kazi ya utumishi wa umma wanafaa kufanya kazi kama fisi,” alisema punde baadaye kauli hiyo ikasambaa kama moto jangwani.

Wakili Miguna Miguna amesikitikia uwezo wa Naibu Rais wa mawasiliano akidokeza anahitaji masomo mapana ya mawasiliano.

Bw Miguna amerejelea wahusika katika masimulizi ya Kiafrika ambayo hutumia fisi kudhihirisha ulafi na ujinga.

“Wanaotoa mfano wa bidii na umoja ni nyuki na mchwa. Rafiki yangu, Rigathi Gachagua, anahitaji masomo mapana ya mawasiliano,” alisema Bw Miguna kwenye mtandao wa X.

Sehemu ya Wakenya hata hivyo wameonekana kuunga mkono kauli ya Naibu Rais wakirejelea kuwa kuna misemo katika jamii ya Agikuyu inayotaja fisi kuwa mchapakazi.

“Pengine shida inatokea katika tafsiri kwa sababu kuna tashbihi ya Kikuyu inayosema, ‘kuruta wira ta hiti’ (kufanya kazi kama fisi). Ila sioni kama ina maana hata hivyo,” alisema Anthony Gichane kwenye X.

“Msemo ‘hiti ya wîra’ ni kauli ya jamii ya Agikuyu ambayo humaanisha bidii. Vyombo vya habari vinatafsiri moja kwa moja ambayo inabadilisha maana,” mtumiaji mwingine wa mtandao wa kijamii Alex Muturi alitoa maoni.

  • Tags

You can share this post!

Miguna: Ruto ameniacha mataani licha ya kuniomba msamaha...

Waislamu mjini Eldoret wakerwa na kauli ya Papa Francis ya...

T L