• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 3:41 PM
Usifakamie mlo tu kujaza tumbo – mtaalamu

Usifakamie mlo tu kujaza tumbo – mtaalamu

NA LABAAN SHABAAN

KAMA ilivyo desturi kila msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya, watu hupumzika na kuchangamkia mapochopocho kochokocho.

Yamkini wengi waliokuwa wakifanya mazoezi ya viungo wataishia kupumzika huku wakipatia ‘mwili shukurani na pole’ na kusahau kutunza afya zao wasinenepe kupindukia, afya ikazorota.

Mtaalamu wa Lishe Bora Dkt Peter Kiarie anashauri kuwa kuheshimu mfumo wa lishe bora kunafaa kuwa hitaji la kila siku.

“Katika msimu wa Krismasi na kukaribisha Mwaka Mpya, watu wanafaa kuwa makini na kile wanachokula kwa kuweka zingatio katika thamani na kiasi cha mlo,” asema Dkt Kiarie.

Akieleza umuhimu wa kufanya mazoezi licha ya watu kuwa likizoni pasi na kuwa na hamkani za kawaida kazini, Dkt Kiarie anasisitiza ni njia bora ya kuwa makini na uzani na afya.

Sherehe zinapokuja na zawadi pamoja na chakula, ni rahisi mtu kusahau mtindo wa lishe bora na shughuli bora za kiafya ambazo amekuwa akifuata mwaka mzima.

Sahani za pishi la pilau na nyama katika kituo cha Afya ya Akili kilichoko Miritini katika Kaunti ya Mombasa mnamo Desemba 25, 2023. PICHA | KEVIN ODIT

Mtaalamu huyu anaelekeza watu waone sikukuu kama siku nyingine zozote za mwaka lijapo suala la ufuataji wa mpangilio wa mlo.

Pia anaonya dhidi ya kujinyima chakula ili uhifadhi pesa kwa ajili ya shamrashamra hizo.

“Katika msimu wa sherehe ni muhimu kuangalia hali yako ya afya. Kwa mfano, kama una anemia, kisukari, magonjwa ya figo na tumbo, lazima uwe mwangalifu na unachokula kama kawaida,” anashauri.

Dkt Kiarie anaeleza kuwa ni muhimu mja kula asilimia 20 ya stachi, asilimia 30 ya protini kama vyakula vya baharini na mayai, na asilimia 50 ya mboga na kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi.

Daktari huyu anaonya dhidi ya hatari zinazowakabili wasiokuwa makini na utaratibu wa lishe akisema wanafaa kutahadhari magonjwa ya kunenepa kupindukia, kisukari, shinikizo la damu, na udhaifu wa kinga mwilini.

Pia anatahadharisha kina mama wanaonyonyesha dhidi ya kupoteza umakini akisema ikitokea hivyo, kuna hatari ya kuathiri ubora wa maziwa.

  • Tags

You can share this post!

Hakikisha raia wana noti mfukoni, Rais aambiwa

Mungai Eve, Trevor wanusurika kwenye ajali

T L