• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Hakuna sherehe za pombe haramu

Hakuna sherehe za pombe haramu

Na TITUS OMINDE

POLISI katika kaunti ya Uasin Gishu wamesitisha sherehe za Krismasi na mwisho wa mwaka zinazoadhimishwa kwa karamu ya pombe haramu kama vile Busaa, muratina na chang’aa kufuatia msako mkali dhidi ya pombe hiyo msimu huu wa sherehe.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Ayub Gitonga alisema polisi wataendelea na msako katika maeneo mbalimbali kwa biashara ya pombe haramu katika kaunti hiyo ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa pombe haramu hawatengeneze pombe hiyo msimu wa sherehe ambapo wao huandaa na kutumia pombe haramu.

Bw Gitonga alisema pombe haramu imeharibu familia nyingi katika kaunti hiyo huku kaunti Ndogo ya Turbo ikiongoza kwa biashara hiyo. ‘Bia haramu imeharibu familia nyingi, waraibu hawawezi kuendelea na majukumu yao ya kawaida. Hii ndiyo sababu sote tunafaa kushikana mikono ili kumaliza pombe hiyo haramu,” Bw Gitonga alisema.

Bw Gitonga alitoa wito kwa umma kutoa habari kuhusu mtu yeyote anayehusika na pombe haramu katika kaunti hiyo kwa jina la kusherehekea Krismasi na mwisho wa mwaka. Alisema maafisa wa polisi wataendelea na msako wa mara kwa mara kwa lengo la kuwakamata wahusika na kuafikisha mahakamani.

Kutokana na msako huo, kwa wiki moja iliyopita zaidi ya lita 5,000 za pombe haramu zimenaswa huku wafanyabiashara zaidi ya 100 wakishtakiwa mahakamani. Wafanyabiashara wengi waliofikishwa mahakamani walikiri makosa ambapo walitozwa faini ya kati ya Sh 500 hadi 20,000 au kutumikia vifungo mbalimbali jela kulingana na kiasi cha pombe kila mshtakiwa alipatikana nayo.

You can share this post!

Mahakimu na majaji hawajapokea nyongeza za mishahara

4 waaga ajali zikiendelea kuongezeka

T L