• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Haya ndiyo mafanikio ya Kenya Kwanza, Rais Ruto aambia Wakenya ‘tuko sawa’

Haya ndiyo mafanikio ya Kenya Kwanza, Rais Ruto aambia Wakenya ‘tuko sawa’

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amesema Kenya iko kwenye mkondo mzuri wa ukuaji kutokana na utekelezaji wa sera za utawala wake mwaka mmoja baada ya kuingia mamlakani.

Akitoa hotuba bungeni mnamo Alhamisi kuhusu Hali ya Taifa, Dkt Ruto alisema mageuzi na mipango ambayo serikali yake inatekeleza katika sekta mbalimbali yameanza kuzaa matunda.

“Tulianza kutekeleza ajenda yetu ya ufufuaji wa uchumi kuanzia ngazi za chini katika mazingira yenye changamoto kadha humu nchini na kimataifa. Lakini mipango yetu katika sekta za Kilimo, Afya, Elimu miongoni mwa zingine imeanza kuleta afueni kwa raia,” akasema.

Rais Ruto alieleza kuwa serikali yake haswa imewekeza katika sekta ya kilimo kama njia mwafaka ya kudhibiti kupanda kwa gharama ya maisha.

“Mpango wa serikali hii wa kupunguza bei ya mbolea kutoka Sh7,000 hadi Sh2,500 kwa gunia moja la kilo 60 sasa umewaweza wakulima kuimarisha uzalishaji wa chakula. Hii ndio maana sasa bei ya unga wa mahindi imeshuka kutoka Sh230 kwa paketi moja ya kilo mbili mwaka 2022 hadi Sh145, kwa kutegemea chapa ya unga ambao utanunua. Na mkebe mmoja wa kilo mbili wa mahindi ile inayojulikana kama gorogoro sasa inauzwa kwa kati ya Sh60 na Sh100,” Rais Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa alisema ni kutokana na hali hiyo ambapo Wakenya wameweza kuongeza uwezo wao wa kuweka akiba.

“Kwa mfano, wale ambao wameajiriwa wamefanikiwa kuweka akiba ya Sh6.5 bilioni kila mwezi kupitia hazina ya NSSF, pesa ambazo bila shaka zitawasaidia kujiimarisha kimaisha,” akasema katika kikao hicho cha pamoja cha wabunge na maseneta.

Hata hivyo, ongezeko hilo la kiwango uwekaji akiba unatokana na hatua ya serikali ya Rais Ruto ya kuongeza makato kwa hazina hiyo ya uzeeni kutoka Sh200 kila mwezi hadi Sh2,000.

Aidha, Rais Ruto alisema serikali yake imepiga jeki wafanyabiashara wadogo kwa mkopo wa gharama nafuu kupitia Hazina ya Hasla.

“Kufikia mwezi Oktoba, Hazina ya Hasla imetoa mikopo ya kima cha Sh36.6 bilioni huku wafanyabiashara hao wadogo wakiweka akiba ya Sh2.3 bilioni. Jumla wafanyabishara 7.5 milioni wamechukua mkopo huo zaidi ya mara moja huku kiwango cha ulipaji kikiwa asilimia 75,” akasema.

Chini ya mpango wa serikali yake ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, Rais Ruto alisema jumla ya nyumba 46,792 zimejengwa kufikia sasa.

“Na nyumba nyingine 40,000 zitaanza kujengwa hivi karibuni kote nchini. Aidha, tunajenga masoko 400 katika katika mpango unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa za serikali za kaunti,” Dkt Ruto akaeleza huku akiongeza mpango huo umezalisha zaidi ya nafasi 50,000 za ajira.

Katika sekta ya elimu, Rais alisema serikali yake imejitolea kutekeleza mageuzi yote yaliyopendekezwa na jopo kazi lililoongozwa na Profesa Raphael Munavu.

“Tumeajiri jumla ya walimu 56,796, idadi kubwa zaidi kuwahi kuajiriwa kwa wakati moja na Mheshimiwa Omboko Milemba hapa anaweza kuthibitisha hilo. Aidha, tumetoa mafunzo zaidi kwa walimu 8,200 watakaofunza katika kiwango cha sekondari ya msingi (JSS),” Dkt Ruto akaeleza.

Aliongeza kuwa mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu utawezesha wanafunzi kutoka jamii masikini kupata elimu hiyo sawa na wengine kutoka jamii zenye uwezo.

“Vile vile, mpango huu utasaidia kuondoa vyuo vyetu vikuu kutoka lindi la madeni ambayo wakati huu yamefikia kima cha Sh60 bilioni,” Rais Ruto akasema.

Katika sekta ya afya, kiongozi wa taifa alisema serikali imeajiri jumla ya wahudumu wa afya katika jamii (CHPs) 100,000.

“Wahudumu hao wamepewa vifaa vyote hitajika na watakuwa wakizunguka kote vijijini kutoa ushauri na huduma za afya msingi,” akaeleza.

Kuhusu usalama, Rais Ruto alisema serikali yake itaendeleza mipango yake ya kupambana na aina mbalimbali za uhalifu kote nchini.

“Tayari juhudi zetu za kupambana na ugaidi, ujangili, na wizi wa mifugo katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya, Kaskazini mwa Bonde la Ufaa na Pwani zimeanza kuzaa matunda,” akasema.

Rais alisema serikali yake inatekeleza mpango ambapo vijana wa Huduma ya Kitaifa (NYS) ndio watapewa kipaumbele katika usajili wa maafisa wa vikosi mbalimbali vya polisi na jeshi.Rais Ruto pia alisema kuwa serikali yake imepiga hatua kubwa zaidi katika mpango wake wa kukumbatia mfumo wa kidijitali kuimarisha utoaji huduma.

“Kufikia sasa jumla ya huduma 13,000 za serikali zinatolewa kwa mfumo ya kidijitali na kufikia Desemba huduma zote zitatolewa kwa mfumo huo,” akaeleza.

Kuhusu mahusiano ya kimataifa, Rais alisema Kenya inashiriki katika michakato ya kuleta amani katika mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan.

  • Tags

You can share this post!

Seneta Karen Nyamu asimulia jinsi penzi lake kwa Samidoh ni...

Washukiwa 14 wanaswa Njiru maafisa wakifanikiwa kutwaa...

T L