• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Hofu wakazi wa Kanagoni wakiamriwa wahame la sivyo wachinjwe

Hofu wakazi wa Kanagoni wakiamriwa wahame la sivyo wachinjwe

NA ALEX KALAMA

SUALA la watu kuaga dunia Shakahola kwa kufuata mafundisho ya kidini ya kupotosha likiendelea kugonga vichwa vya vyombo vya habari, wakazi wa kijiji cha Majengo, Kanagoni katika eneobunge la Magarini wanaishi kwa hofu na mahangaiko baada ya kutishiwa wahame la sivyo wachinjwe.

Shakahola na Kamagoni ni maeneo yanayopatikana eneobunge la Magarini katika Kaunti ya Kilifi.

Kufikia Jumapili, takriban wakazi 260 kutoka kijiji cha Majengo walikuwa wameachwa bila makao baada ya makazi yao kubomolewa na bwanyenye mmoja anayedai kumiliki kipande hicho cha ardhi.

Wakiongozwa na mzee wa kijiji eneo hilo Kalume Kazungu, wakazi hao wanadai kuwa ubomoaji wa makazi yao ulifanyika chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi bila ya wao kupewa ilani ya kuhama eneo hilo.

“Hatuna makao hata saa hii tunavyoongea tumelala nje tukipigwa na baridi. Watoto hawawezi kuenda shule kwa sababu nguo zote zilichomwa na wanaonyemelea hii ardhi yetu wakidai ni yao. Sisi maisha yetu yote tumeishi hapa hadi tuko na watoto na wajukuu lakini leo hii tunakuja kuambiwa tuondoke eti hapa sio kwetu bali ni pa mwenyewe,” akasema Bw Kazungu.

Alikuwa na machungu sana.

“Tafadhali viongozi wetu… gavana wetu Gideon Mung’aro… tunaomba utuangalie mahali hapa ili nasi tuweze kupata haki katika hili suala ambalo limetuandama maana tunaumia. Watu wamekuja na polisi wakiwa wanaongozwa ni Mkuu wa Polisi wa ADU na mkubwa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Marereni na kubomoa nyumba zetu huku wakiteketeza baadhi ya nyumba zenyewe. Sasa tunalala nje,” alisema Bw Kazungu.

Bw Kazungu anasema kuwa wamekuwa wakipitia changamoto nyingi tangu ubomoaji huo ufanyike.

“Hapa ndani tuko watu zaidi ya 260 ambao tumezungukwa na huyu bwanyenye ambaye anaitwa Salat… tuko na familia zetu, tuko na mifugo yetu, tuko na mimea yetu, tuko na mashamba yetu tunafanya maendeleo. Iweje mtu atoke huko bara aje atutatize na kutufurusha kwetu akisema ni kwake? Umri huu niliofika wa miaka 70 unifukuze kwangu unataka niende wapi?” akauliza.

Nyuma ya nyumba mojawapo ya zilizobomolewa Kanagoni kuna mashamba yenye mimea ya chakula inayostawi vyema. PICHA | ALEX KALAMA

Kwa upande wake Kadzo Msanzu, ameambia Taifa Jumapili kuwa wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa watu ambao wamekuwa wakitekeleza ubomoaji huo wa nyumba. Bi Msanzu amedai watu hao walitishia kuwaua kwa kuwachinja wakikataa kuondoka kwenye kipande hicho cha ardhi.

“Tumekuwa tukitishwa kila wakati tukiambiwa tuhame hapa la sivyo tutauawa. Sasa tuhame tuende wapi na hapa ndio kwetu? Kama mimi nimezaliwa hapa nimekulia hapa na nimeolewa eneo hili. Isitoshe, mume wangu aliaga dunia na niko na watoto watano ambao wananitegemea mimi… ukinifukuza hapa unataka niende wapi na sina pa kuenda?” akasema Bi Msanzu akiomba serikali na viongozi wa Kilifi waingilie kati kuwasaidia.

Juhudi za Taifa Jumapili za kutaka kuongea na afisa mkuu wa polisi eneo la Adu Ayubu Abdi ziligonga mwamba baada ya afisa huyo kukosa kuchukua simu tulipompigia.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume adaiwa kulawiti vijana wanne mjini Kilifi

Manchester City watia kibindoni tuzo ya Sh12.7 bilioni

T L