• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
Manchester City watia kibindoni tuzo ya Sh12.7 bilioni

Manchester City watia kibindoni tuzo ya Sh12.7 bilioni

Na MASHIRIKA

SUBIRA ya muda mrefu ya Manchester City kutawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza katika historia ilifikia kikomo mnamo Jumamosi usiku baada ya kupokeza Inter Milan kichapo cha 1-0 kwenye fainali iliyochezewa jijini Istanbul, Uturuki.

Ushindi huo uliowazolea kima cha Sh12.7 bilioni, uliwezesha masogora hao wa mkufunzi Pep Guardiola kukamilisha kampeni za msimu huu wa 2022-23 wakijivunia mataji matatu, likiwemo Kombe la FA na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Ni ufanisi ulioshuhudia miamba hao wakifikia rekodi ya Manchester United waliotia kibindoni mataji matatu – FA, EPL na UEFA mnamo 1999. Man-City sasa ndicho kikosi cha nne baada ya Liverpool, Man-United na Chelsea kuwahi kujizolea ubingwa wa UEFA kutoka Uingereza. Hakuna taifa jingine la bara Ulaya ambalo limewahi kutoa zaidi ya washindi watatu tofauti wa taji la UEFA.

Licha ya kutokuwa katika ubora wao na kupoteza maarifa ya kiungo Kevin de Bruyne katika kipindi cha kwanza, Man-City walihimili vilivyo makali ya Inter waliocheza kwa uangalifu mkubwa. Hata hivyo, ngome ya mabingwa hao wa Coppa Italia waliopoteza nafasi za wazi kupitia kwa Lautaro Martinez, Federico Dimarco na Romelu Lukaku, ilifumuliwa na Rodri Hernandez aliyeachilia fataki katika dakika ya 68.

Taji hilo la UEFA lilikuwa la tatu kwa Guardiola kujitwalia katika historia yake ya ukufunzi. Kocha huyo raia wa Uhispania aliwahi kutwaa mataji mengine mawili ya kipute hicho akidhibiti mikoba ya Barcelona (2009, 2011). Anatarajiwa kuongoza waajiri wake kujumuika na maelfu ya mashabiki kwenye barabara za jiji la Manchester kusherehekea mafanikio yao ya kihistoria muhula huu.

Man-City walitinga fainali ya UEFA muhula huu baada ya kudengua waliokuwa mabingwa watetezi Real Madrid kwa kichapo cha jumla ya mabao 5-1 kwenye nusu-fainali huku Inter wakibandua AC Milan kwa magoli 3-0.

Hadi kufikia msimu wa 2020-21 ambapo masogora wa Guardiola walikomolewa na Chelsea kwenye fainali ya UEFA, Man-City hawakuwa wamewahi kuvuka zaidi ya hatua ya robo-fainali kwenye kipute hicho licha ya kujivunia maarifa ya Guardiola aliyetua Etihad mnamo 2016.

Chelea walitandika Man-City 1-0 kwenye fainali ya UEFA mnamo Mei 2021 katika uwanja wa Estadio do Dragao jijini Porto, Ureno, kabla ya Real Madrid kuwadengua kwenye nusu-fainali za 2021-22.

Mechi dhidi ya Inter ilikuwa ya nne kati ya nane kwa Man-City kushinda ugenini. Awali, miamba hao walikuwa wameshindwa kutamba dhidi ya Real na Bayern ugenini kabla ya kuangushwa pia na Brentford kwa 1-0 mnamo Mei 28, siku tatu baada ya Brighton kuwalazimishia sare ya 1-1 katika EPL ugani Amex.

Hata hivyo, walijinyanyua upesi na kucharaza Man-United 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Juni 3 ugani Wembley, Uingereza. Man-City sasa wamefunga katika kila mojawapo ya mechi nane zilizopita za UEFA na wamejizolea taji hilo msimu huu bila kupoteza pambano lolote la kipute hicho.

Kombe la EPL ambalo Man-City walijitwalia msimu huu lilikuwa lao la tatu mfululizo huku la FA likiwa la kwanza tangu 2009 walipoponda Watford 6-0. Chini ya Guardiola, Man-City wametawazwa mabingwa wa EPL mara tano katika kipindi cha misimu sita iliyopita.

“Inaridhisha kwamba ndoto yetu imetimia. Kikosi kimekomaa na tunalenga kufanya ushindi wa mataji kuwa sehemu ya desturi yetu,” akasema Guardiola.

“Ilipendeza sana kuhifadhi ubingwa wa EPL, ilifurahisha mno kutwaa Kombe la FA na sasa tumezoa UEFA kwa mara ya kwanza katika historia,” akaongezea.

Mnamo 2019, Man-City waliweka rekodi ya kuwa kikosi cha nane katika soka ya Uingereza; na cha kwanza baada ya Chelsea mnamo 2009-10 kujizolea EPL, Carabao Cup na Kombe la FA. Mabingwa hao mara tisa wa EPL sasa wamenyanyua mataji 12, yakiwemo matano ya EPL tangu 2016.

“Kunyanyua mataji 12 chini ya miaka sita si jambo jepesi. Ushindi huu wa UEFA una maana kubwa mno kwa kila mmoja wetu. Huu ni msimu ambao sitawahi kusahau maishani,” akasema nahodha Ilkay Gundogan.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Hofu wakazi wa Kanagoni wakiamriwa wahame la sivyo wachinjwe

Ruto anavyomdhibiti Gachagua

T L