• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Idadi ya watu waliothibitishwa kufariki Shakahola yagonga 326

Idadi ya watu waliothibitishwa kufariki Shakahola yagonga 326

NA ALEX KALAMA 

MAAFISA wanaoendeleza shughuli ya ufukuaji wa makaburi ili kutoa miili ya watu waliozikwa katika hali tatanishi kwenye msitu wa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi mnamo Alhamisi wamefanikiwa kufukua miili minane na kufikisha idadi ya jumla ya miili iliyofukuliwa eneo hilo kuwa 326. 

Katika taarifa yake ya kila siku kwa vyombo vya habari mshirikishi wa Pwani Rhoda Onyancha amesema hakuna mtu aliyekamatwa leo Alhamisi katika msitu wa Shakahola kwenye operesheni inayoendelea na ambayo pia inalenga kuwasaka manusura waliosalia ndani ya chaka hilo la mauti.

“Siku ya leo tumepata miili minane baada ya kufukua makaburi katika msitu na kufanya idadi jumla ya watu waliofariki kuwa 326 huku idadi ya  waliokamatwa kufikia sasa ikisalia kuwa watu 36,” amesema Bi Onyancha.

Bi Onyancha ameeleza kuwa kufikia sasa, idadi ya watu waliookolewa kwenye msitu huo wa Shakahola imesalia 95 huku watu 93 wakiwa wamechukuliwa chembechembe za DNA kwa uchunguzi zaidi.

“Kufikia sasa watu 19 wameunganishwa na jamaa zao huku idadi ya watu walioripotiwa kupotea ikiwa bado ni ile ya watu 613,” amesema Bi Onyancha.

Mnamo Jumatano maafisa walifanikiwa kufukua miili 15.

Aidha afisa huyo wa utawala amesema shughuli ya ufukuaji wa makaburi ili kutoa maiti za wahanga wa imani potovu bado inaendelea katika msitu huo.

  • Tags

You can share this post!

Bajeti 2023/24: Waziri Ndung’u asema ni heri sukari...

Tuwei amezea mate kiti cha naibu rais wa Shirkisho la...

T L