• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Jambazi wa kuwekea walevi mchele ashtakiwa kwa wizi wa sh1.4 milioni

Jambazi wa kuwekea walevi mchele ashtakiwa kwa wizi wa sh1.4 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME anayedaiwa kuwa mwanachama wa kundi la majambazi wanaowekea watu dawa za kulevya kwenye pombe almaarufu “mchele” ameshtakiwa kwa kumpumbaza mfanyabiashara na kumwibia pesa Sh1.15 milioni.

Mbali na pesa alizomwimbia Paul Muingo katika benki ya Absa tawi la Juja kaunti ya Kiambu, Ibrahim Mwangi Kiria pia alishtakiwa kwa kuiba kadi za benki (ATM), saa ya mkono na simu mbili.

Ibrahim Mwangi Kiria alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina.

Hata hivyo Kiria alikanusha mashtaka manne dhidi yake kisha kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda akaomba kesi hiyo iunganishwe na nyingine ambapo Everlyne Wambui Mutura, Janet Wanjiru Ngugi na David Kariuki Wanjao walishtakiwa wiki iliyopita kwa makosa hayo.

Kiria aliagizwa azuiliwe hadi leo (Aprili 19,2023) atakaporudishwa kortini kesi inayowakabili Wambui, Wanjiru na Kariuki itakapotajwa kutengewa siku ya kusikizwa iunganishwe na yake.

Kiria anadaiwa alitekeleza uhalifu huo usiku wa Machi 20/21,2023 katika kilabu cha DJ Club kilichoko kwenye makutano ya barabara ya Thika Road na Kimbo.

Kiria anakabiliwa na mashtaka ya kula njama za kuiba Sh1, 154, 081, simu tatu muundo wa Samsung za thamani ya Sh155,000 kadi za ATM za benki ya Absa, saa ya mkono ya thamani ya Sh150,000 na kitambulisho cha Paul Maingo.

Thamani ya vyote alivyoporwa Paul Muingo inakadiriwa kuwa Sh1, 459, 081.

Mshtakiwa huyo pia anakabiliwa na shtaka lingine la kumpumbaza Paul Maingo kwa kumwekea kileo katika pombe usiku wa Machi 20/21, 2023 katika kilabu cha DJ Club.

Katika Benki ya Absa tawi la Juja Kiria anakabiliwa na shtaka la kumwibia Paul Muingo Sh1, 154, 081.

Mahakama ilifahamishwa kwamba mshtakiwa alishiriki katika uhalifu wa wizi, kunywesha watu dawa ya kuwapumbaza kwa lengo la kuwaibia.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana lakini Bw Gikunda akapinga akisema “azuiliwe hadi leo (Aprili 19,2023) kesi yake iunganishwe na nyingine.”

Akitoa uamuzi Bw Onyina aliamuru mshtakiwa azuiliwe gerezani hadi leo kesi inayomkabili iunganishwe na nyingine itakayotengewa siku ya kusikizwa.

Akimweleza mshtakiwa kwa lugha ya Kiswahili Bw Onyina alifafanua, “nimesikiza mawasilisho ya kiongozi wa mashtaka na nimefikia uamuzi utazuiliwa rumande hadi Aprili 19, 2023 kesi hii inayokukabili iunganishwe na nyingine.”

  • Tags

You can share this post!

Muziki: Wakili Angela Ndambuki aling’ara sana na...

Ashtakiwa kwa vitisho vya kuua

T L