• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
Kampuni ya mradi wa kupunguza gesi ukaa yamulikwa kwa kunyanyasa wanawake kingono

Kampuni ya mradi wa kupunguza gesi ukaa yamulikwa kwa kunyanyasa wanawake kingono

NA LUCY MKANYIKA

RIPOTI ya mashirika yasiyo ya kiserikali imemulika kampuni ya Wildlife Works, inayoendesha mradi wa kupunguza kaboni katika Kaunti ya Taita Taveta, kwa ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wafanyakazi wa kike na jamii ya eneo hilo kwa upana.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Utafiti wa Mashirika ya Kimataifa (Somo) na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), ilionyesha kuwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo inayoshirikiana na shirika la Verra katika mradi huo wa Kasigau Corridor REDD+, wamekuwa wakinyanyasa wanawake kimapenzi.

Mradi huo ulikusudia kulinda misitu na wanyamapori, kupunguza utoaji wa gesi ukaa, na kutekeleza miradi ya manufaa kwa jamii na hivyo kutoa ajira, elimu, na uwezeshaji wa wanawake.

Mradi huo ni mmojawapo wa miradi iliyoidhinishwa kukabiliana na kaboni duniani na umepokea sifa kwa kufanikisha maendeleo endelevu na umeuza kaboni kwa Microsoft, Shell, Benki ya Dunia (WB), na Benki ya Uwekezaji wa Ulaya.

Hata hivyo, ripoti hiyo imefichua unyanyasaji wa kijinsia ambao umekithiri katika eneo hilo la mradi la Kasigau.

Ripoti hiyo inaonyesha jinsi baadhi ya wafanyakazi wa kiume na walinzi wa wanyamapori (rangers) walivyonyanyasa kingono wafanyakazi wa kike, wanawake na wasichana wa eneo hilo, ili kupewa kazi, kupandishwa vyeo au kuongezwa marupurupu.

Walinzi wa wanyamapori wanaofanyia Wildlife Works kazi. PICHA | HISANI

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa walioasi walipokea vitisho na ubaguzi hadi kwa familia zao.

“Utafiti wetu unaonyesha kuwa unyanyasaji huu umeendelea kwa kipindui cha mwongo mmoja au zaidi,” inasema.

Waathiriwa pia walikabiliwa na vikwazo wakati wa kuripoti unyanyasaji huo, kama vile unyanyapaa na kukosa kupata haki.

“Wanawake waliokataa unyanyasaji wa kingono waliishi na kufanya kazi kwa uoga, kama mmoja wao alivyosema kwa sababu wanaweza kuachishwa kazi wakati wowote bila sababu za kimsingi,” ripoti hiyo ilisema.

Ripoti hiyo ilitoa wito kwa kampuni hiyo ya Wildlife Works, wateja wake, na kampuni ya ukaguzi kushughulikia madai hayo ya waathiriwa na jamii kwa ujumla na kuchukua hatua za kuzuia na kurekebisha ukiukaji wowote zaidi dhidi ya haki za binadamu.

Ripoti hiyo pia inaitaka serikali kuwajibika kuhakikisha kuwa haki za watu walioathirika zinaheshimiwa na kulindwa na wahusika wanachukuliwa hatua.

Kwa upande wake, shirika la Verra lilisema kuwa limefahamishwa kuhusu tuhuma za unyanyasaji wa kimapenzi katika Mradi wa Kasigau. Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Maswala ya Mawasiliano na Utetezi Joel Finkelstein alisema shirika hilo linachukua hatua kwa kuanzisha uchunguzi dhidi ya madai hayo.

“Verra ilifahamishwa kuhusu tuhuma za unyanyasaji wa kingono katika Mradi wa Kasigau nchini Kenya. Verra itachukua hatua mara moja,” ilisema taarifa hiyo ya Finkelstein.

Alisema mradi huo utasitishwa hadi uchunguzi utakapokamilika.

Naye Rais wa Wildlife Works Mike Korchinsky alisema katika taarifa kwamba hatua ilichukuliwa baada ya ripoti ya madai hayo kufichuka.

“Wafanyikazi wawili waliotajwa wamesimamishwa kazi na mfanyakazi mwingine angali anachunguzwa huku matokeo ya uchunguzi huo yakisubiriwa,” alisema Korchinsky.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya alaani hatua ya KRA kumpokonya marashi katika uwanja...

Serikali yaonya wakuu shuleni dhidi ya kuongeza karo

T L