• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
KCSE: Kinaya cha walimu wengi kumulikwa kwa udanganyifu waziri Machogu akisisitiza ‘tuko tu sawa’

KCSE: Kinaya cha walimu wengi kumulikwa kwa udanganyifu waziri Machogu akisisitiza ‘tuko tu sawa’

NA CHARLES WASONGA

WALIMU wakuu wa shule tisa za upili na walimu 23 wamesimamishwa kazi kwa madai ya kushiriki udanganyifu katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoendelea kote nchini.

Aidha, watahiniwa 46 wamepatikana na hatia hiyo ya kujaribu kutumia njia za mkato kupita mtihani huo ambao utaamua ikiwa watajiunga na vyuo vikuu na vile vya kadri mwaka 2024.

Miongoni mwa walimu hao wakuu ni Charles Onyari wa Shule ya Upili ya Nyambaria iliyoko katika Kaunti ya Nyamira, aliyesimamishwa kwa madai ya kupatikana akishiriki uovu huo ilhali alikuwa msimamizi wa kituo cha mtihani.

Shule hiyo ya kitaifa, isiyojulikana sana, ilishangaza wengi kwa kuongoza katika matokeo ya KCSE 2022 kwa kupata alama wastani ya 10.60.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu anasema kuwa visa nyingi vya uovu huo mwaka huu 2023 viliendeshwa kwa njia ya kuingiza vitu visivyohitajika ndani ya vyumba vya kufanyia mitihani, watu kujifanya kuwa watahiniwa na wasimamizi kuwasaidia watahiniwa.

“Kufikia sasa tumethibitisha visa vitatu vya watahiniwa kushirikiana, visa viwili vya watu kujaribu kujifanya kuwa watahiniwa na mameneja tisa ambao ni walimu wakuu waliokuwa wakisimamia shule mbalimbali wamesimamishwa kazi. Aidha watahiniwa 46 wametuhumiwa,” waziri Machogu akasema Ijumaa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kolanya, iliyoko Teso Kaskazini, Kaunti ya Busia. Shule hiyo ni ya hadhi ya kitaifa.

Mwalimu Mkuu mwingine aliyesimamishwa kazi kwa wizi wa mtihani ni Eva Odhiambo wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Sironga, iliyoko Kaunti ya Nyamira.

Shule nyingine ambako wizi wa mitihani iliripotiwa ni Shule ya Upili ya Gekomoni na Shule ya Upili ya Wavulana ya St Paul Gekano, zote katika Kaunti ya Nyamira.

Katika Kaunti ya Migori, polisi walitibua sakata ya wizi wa mitihani na kuwakamata walimu 23 wanaozuiliwa kuhojiwa.

Baadhi ya walimu walikamatwa katika kanisa moja Kaunti ya Migori wakiandaa majibu ya maswali ya mtihani wa Kemia kwa nia ya kupitisha majibu kwa watahiniwa wa Shule ya Upili ya Wasichana ya St Mary’s Mabera.

  • Tags

You can share this post!

Cameroon yaizidi Kenya maarifa katika mechi ya kufuzu Kombe...

Mke wa mwanasoka Ezekiel Otuoma adhihirisha mapenzi ya...

T L