• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kero ya kukosa matawi ya benki visiwani

Kero ya kukosa matawi ya benki visiwani

NA KALUME KAZUNGU

UKOSEFU wa matawi ya benki kwenye visiwa vya Lamu Mashariki umewasukuma wenyeji kugeukia mbinu za zamani za kuhifadhi hela, ikiwemo kuchimba mashimo na kuzificha ndani ya majumba yao.

Kuna wengine ambao wamekuwa wakificha mkwanja chini ya mito ilhali kunao wanaotumia mikebe na nyungu maalum kuhifadhi pesa.

Kaunti ndogo ya Lamu Mashariki ina ukubwa wa karibu nusu ya kaunti nzima ya Lamu, japo idadi ya watu wanaoishi eneo hilo ni finyu.

Lamu Mashariki ni eneo linalojumuisha karibu visiwa 15 kati ya 35 vipatikanavyo kaunti ya Lamu.

Miongoni mwa visiwa vipatikanavyo Lamu Mashariki ni Faza, Kizingitini, Siyu, Ndau, Kiwayu, Mkokoni, Kiunga, Pate, Tchundwa, Mbwajumwali, Mtangawanda, Shanga, Rubu na viunga vyake.

Kisiwa cha Mtangawanda kilichoko Lamu Mashariki. Eneo hilo halina tawi lolote la benki. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kulingana na sensa ya mwaka 2019, Lamu ina jumla ya watu 143,920 ambapo zaidi ya watu 22,000 wanapatikana Lamu Mashariki ilhali idadi iliyobakia ikipatikana Lamju Magharibi.

Licha ya watu kuishi Lamu Mashariki, ikiwemo wafanyakazi wa umma, eneo hilo halijawahi kuwa na tawi lolote la benki.

Wakazi wanaohitaji huduma za benki eneo hilo hulazimika kukodisha boti ya kibinafsi kwa kati ya Sh15,000 hadi Sh20,000 kusafiri masafa marefu ndani ya Bahari Hindi hadi kisiwani Lamu kupata huduma hizo.

Aidha kwa wale wanaosafiri wakitumia mashua za usafiri wa umma, wao huishia kutumia kati ya Sh2000 hadi Sh3,000 kufika kisiwa cha Lamu kupata huduma za benki na kurudi.

Ikumbukwe kuwa wakazi wengi wanaoishi Lamu Mashariki ni wavuvi ambao mara nyingi hupata fedha nyingi kutokana na mauzo ya samaki.

Kwa mfano, katika kisiwa cha Kizingitini ambacho ndicho chenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi Lamu Mashariki, wavuvi hupata hadi Sh1 milioni kwa siku kutokana na mauzo ya samaki, hasa kambakoche (lobster).

Kisiwa hicho aidha hakina benki yoyote.

Kisiwa cha Faza ambacho ndicho makao makuu ya Lamu Mashariki pia kinakosa tawi lolote la benki licha ya hadhi kinayobeba.

Hapa, muungano mmoja wa wavuvi (BMU) hupata hadi Sh5 milioni kila mwezi kutokana na mauzo ya samaki.

Akizungumza na Taifa Leo, mzee wa Kizingitini, Khaldun Vae alisema ukosefu wa benki umewaacha wengi wakitumia mbinu walizoridhi karne za mababu zao katika kuhifadhi na kuwekeza.

Lamu Mashariki ni ngome kuu ya Waswahili wa asili yua Wabajuni.

“Sisi Wabajuni tuko na mbinu zetu za kuhifadhi fedha, ikiwemo kubaini sehemu maalum ya nyumba yako na kuchimba shimo la kuhifadhia fedha zako. Pia kuna wale wanaoficha hela kwenye mito nakadhalika. Haya yote tunayafanya kutokana na ukosefu wa benki maeneo yetu,” akasema Bw Khaldun.

Chifu wa Kizingitini Aboud Luqman alisema ukosefu wa benki umepelekea wakazi kila mara kupoteza hela zao kupitia wizi au majanga ya moto.

Alishikilia haja ya taasisi za kifedha kuzingatia kuanzisha matawi ya benki Lamu Mashariki ili kuwaokoa wakazi kutokana na madhila ya kukosa huduma hizo muhimu.

“Hapa watu wamekuwa wakilengwa na kuibiwa hela majumbani mwao. Utasikia mtu amepoteza Sh100,000 zilizoibwa nyumbani kwake. Kuna wengine huishia kupoteza malaki ya pesa wakati mikasa ya moto inapozuka. Kumbuka nyumba nyingi hapa Kizingitini na Lamu Mashariki kwa jumla paa zake ni zile za kuezekwa kwa makuti,” akasema Bw Luqman.

Khadija Shee aliomba kuwepo na mpango wa benki tofauti tofauti kufungua matawi yake hivi karibuni, akishikilia kuwa kukosekana kwa huduma za benki kunawakosesha amani na usingizi.

“Utalalaje fofofo kwenye nyumba yako ukijua fika kuwa umehifadhi maelfu ya pesa taslimu? Nyakati hizi ngumu za kiuchumi wengi wamekuwa wakilenga watu wenye hela na kuwapora,” akasema Bi Shee.

Ukosefu wa benki aidha umetoa mwanya wa makampuni ya mawasiliano kuvuna pakubwa kwani maajenti wengi wa MPESA wamejawa kwenye visiwa vya Lamu Mashariki.

Kulingana na diwani wa zamani wa Lamu Mashariki Fahd Adnan Dini, ambaye kwa sasa ni diwani maalum katika bunge la Kaunti ya Lamu, eneo lao liko na zaidi ya maajenti 100 wa M-Pesa.

“Hata kama kuna M-Pesa, hiyo haitoshi. Hizi huduma za kifedha za simu zina mipaka. Huwezi kutoa au kuweka hela nyingi kupita mipaka iliyopo. Hii inamaanisha ukitaka kuhifadhi au kutoa fedha nyingi lazima uvuke hadi kisiwa cha Lamu kufanya hivyo. Twahitajki benki karibu nasi,” akasema Bw Dini.

Baadhi ya wafanyakazi wa serikali, ikiwemo walimu, madaktari, wauguzi, polisi na wengineo waliohojiwa na Taifa Leo walitaja ukosefu wa benki eneo hilo kuwa kisirani kwao.

Joseph Menza, ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari ya Siyu, Lamu Mashariki, alisema kupata mkopo wa benki lazima ukwamke kimfuke kukodi boti hadi kisiwa cha Lamu kutafuta mikopo hiyo.

“Wakati unapopatwa na dharura inayohitaji hela za haraka huwa ni kisirani. Tunmalazimika kuvuka bahari kwa boti hadi Lamu kutafuta benki ili ujipatie mkopo. Mwishowe utapata kuwa karibu hela zote za mkopo umezitumia kwa usafiri wa baharini tu ambao ni ghali,” akasema Bw Menza.

Gavana wa Lamu Issa Timamy amekuwa mstari wa mbele kupigia debe taasisi za kifedha kufungua matawi yake Lamu Mashariki ili kuwanusuru watu wake.

“Inasikitisha kuwa karne hii ya 21 watu wangu wa Lamu Mashariki bado hawana huduma za benki. Ni vyema serikali kuu itusaidie kuzungumza na wamiliki wa benki ili kufungua matawi yake kule. Lamu Mashariki pia ni Kenya na wananchi wanahitaji huduma bora,” akasema Bw Timamy.

Kauli yake iliungwa mkono na Waziri wa Biashara na Uwekezaji wa kaunti ya Lamu, Aisha Miraji aliyesisitiza kuwa tayari mazungumzo yanaendelea kati ya ofisi yake na taasisi za kifedha ili matawi ya benki yafunguliwe Faza na sehemu nyingine muhimu za Lamu Mashariki.

  • Tags

You can share this post!

Soka: Green Commandos waapa kurejesha heshima yao

Kijana wa miaka 28 alivyoua babake kinyama Murang’a...

T L