• Nairobi
  • Last Updated June 14th, 2024 1:45 PM
KRA sasa yanyemelea mama mboga na juakali kusaka mabilioni

KRA sasa yanyemelea mama mboga na juakali kusaka mabilioni

NA PETER MBURU

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) imezidisha juhudi zake za kulenga biashara za juakali na kina mama mboga (SMES) huku ikitumai kukusanya karibu Sh2.8 bilioni.

Akizungumza katika Kongamano la Ushuru 2023 linalofanyika kila mwaka, Kamishna Mkuu wa KRA, Humphrey Wattanga alisema Mamlaka hiyo kwa sasa inamulika sekta ya juakali nchini, ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikikwepa kulipa ushuru licha ya kuwaajiri Wakenya wapatao 15 milioni.

Alisema KRA inajishughulisha kutatua changamaoto ambazo zimesababisha idadi kubwa ya SMEs kufungiwa nje ya kitengo kinachotozwa ushuru licha ya kuwa na “uwezo mkuu wa kuchangia mapato ya taifa,” kwa kuwezesha biashara hizo “kuzingatia kanuni za ushuru.”

“Mpango mojawapo chini ya mradi wa KRA wa kuongeza kiwango cha ushuru ni kuvuta sekta ya juakali katika kitengo cha ushuru, idadi kubwa ikiwa biashara ndogondogo na kina mama mboga. Kwa hivyo, kuna haja ya kuunda mikakati na sera za kuiwezesha KRA kujumuisha sekta hii katika kundi la kulipa ushuru,” alisema Bw Wattanga.

KRA inapanga kufanya kazi na Hazina Kuu katika kubuni sera zitakazorahisisha, kuunganisha na kupunguza ada tele za ushuru zinazotozwa sekta ya juakali, alisema Bw Wattanga.

Aliongeza, Mamlaka hiyo itawapa mafunzo wafanyabiashara husika “kuelewa haja ya kulipa ushuru.”

Changamoto

Kauli hii mpya ya KRA inaashiria hatua ya kuendelea kuandama sekta ya juakali inayochukuliwa kuwa ngumu kutoza ushuru na inayokadiriwa kuwa na uwezo kutoa jumla ya Sh2.8 trilioni, kulingana na Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) 2023.

“Sekta ya juakali inaweza kuchangia kiasi cha Sh2, 800 bilioni za ushuru jinsi ilivyoashiriwa na utafiti kuhusu MSME,” ilisema Hazina Kuu.

Karibu wiki tatu zilizopita, KRA iliwatuma maafisa 1,400 wa nyanjani kote nchini kutekeleza majukumu kadhaa ikiwemo, “kuwasaidia walipa ushuru kuweka maelezo yafaayo kwenye akaunti zao za malipo ya ushuru kidijitali, usajili wa biashara ambazo hazijajiandikisha na KRA, ikiwemo kuongeza majukumu husika, kuthibitisha maelezo kama vile eneo, maelezo ya nambari za mawasiliano na kusaidia walipa ushuru kuzingatia kanuni nyinginezo kuhusu ushuru.”

Serikali ya William Ruto imezidi kuandama mapato ya juakali na mama mboga ili kuanza kutoza ushuru sekta hiyo huku iking’ang’ana na bajeti finyu na ahadi kuu za kiuchumi ilizotoa kwa Wakenya.

Mnamo Oktoba 2022, Rais Ruto alisema nambari za KRA ni milioni saba pekee ikilinganishwa na wateja 30 milioni waliojiandikisha na M-pesa, kinaya kinachoashiria kuna uwezekano wa kuvutia walipa ushuru zaidi.

“Hali kwamba fursa hii bado haijajitokeza wazi kwa KRA inaonyesha wazi ni kwa nini mabadiliko ni muhimu. Kila Mkenya aliye na kitambulisho ni sharti awe na nambari ya kulipa ushuru,” alisema Rais.

Wataalamu wa ushuru pia wameelezea kuwepo haja ya serikali kubuni sera zitakazounda mfumo thabiti wa ushuru unaoweza kutabirika.

 

  • Tags

You can share this post!

Wetang’ula alilia ‘Boychild’ kielimu

Kioja mkuzaji bangi akikataa kukamatwa

T L