• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kwa kuua waandamanaji polisi wanatekeleza mauaji ya kimbari – Wandayi

Kwa kuua waandamanaji polisi wanatekeleza mauaji ya kimbari – Wandayi

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya wamesema wanasikitishwa na hatua ya polisi kutumia nguvu kupindukia na hata kuwaua waandamanaji mchana peupe.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi amesema leo Alhamisi ikiwa siku ya pili ya wimbi la tatu la maandamano, tayari wameridhishwa na ufanisi wao na akawapongeza Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi kupinga hatua ya serikali kuongeza ushuru.

Amedai kwamba serikali ya Kenya Kwanza inaongoza kwa udhalimu wa hali ya juu.

Amewapongeza madereva wa malori ya masafa marefu kwa kusitisha shughuli zao ili waandamanaji wapate nafasi ya kutosha.

“Hofu yangu ni kwamba polisi wamepewa maagizo waue waandamanaji, ambao ni Wakenya wazalendo, mchana peupe. Tunaiomba jamii ya kimataifa iangazie udhalimu huu na itoe kauli ya kulaani,” amesema Bw Wandayi.

Ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iwachukulie hatua kali maafisa watakaopatikana na hatia.

Aidha ameiomba Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) ikae macho na ifuatilie kwa makini hali nchini Kenya.

“Haya ni mauaji ya kimbari na uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu. Mashambulio haya yamepangwa na yanawalenga Wakenya wasio na hatia,” amesema mbunge huyo wa Ugunja.

Amesema ni aibu kwa maafisa kuwateka nyara viongozi waliochaguliwa kama Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ambaye hadi kufikia sasa hapatikani kwa simu.

“Badala ya polisi kuwaita na kuwafungulia mashtaka kwa njia ya heshima ikiwa kweli wamekosa, wanatumia mabavu na unyama,” amesema.

Ameahidi kwamba raia watajumuika katika uwanja wa Central Park katikati mwa jiji la Nairobi saa tisa alasiri na hivyo akawataka polisi wawape ulinzi.

Naye Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi amedai wana ushahidi sheria ya Fedha, 2023 inatekelezwa licha ya mahakama kuipiga breki.

Amesema hawezi akazungumzia mengi suala hilo kwa sababu kesi ingali mahakamani.

 

  • Tags

You can share this post!

Wanaharakati wakashifu tukio askari kujifanya mwanahabari...

Rais Ruto kwa Odinga: Sauti ya Wakenya 2022 ilikuwa maamuzi...

T L