• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Wanaharakati wakashifu tukio askari kujifanya mwanahabari kukamata mwandamanaji 

Wanaharakati wakashifu tukio askari kujifanya mwanahabari kukamata mwandamanaji 

NA SAMMY WAWERU

WANAHARAKATI wa kutetea haki za kibinadamu wamekashifu vikali kisa ambapo afisa wa polisi Jumatano, Julai 19, 2023 alijifanya mwanhabari kukamata mwandamanaji. 

Tukio hilo lilifanyika eneo la Mathare, Nairobi wakati wa maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio la Umoja.

Watetezi wa haki za kibinadamu, wakiongozwa na Haki Africa wamesema kisa cha afisa huyo kinahatarisha maisha ya wanahabari.

“Ni hatia na makosa kwa askari kujifanya mwanahabari, kisha anakamata waandamanaji. Tukio la Jumatano, linahatarisha utendakazi wa wanahabari,” akasema Bw Hussein Khalid, Afisa Mkuu Mtendaji Haki Africa, mnamo Alhamisi kwenye kikao na waandishi wa habari Mjini Mombasa.

Kauli ya wanaharakati inawiana na ya Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK), lililotoa taarifa yake kukashifu tukio hilo la Mathare.

Afisa asiye na mavazi rasmi ya polisi, alionekana akinakili video kwa simu akiwa miongoni mwa wanahabari na ghafla akamnyaka mmoja wa waandamanaji aliyekuwa akijibizana na askari.

Ni hatua inayofasiriwa huenda ikahujumu uhuru na utendakazi wa waandishi wa habari, ambao hutangamana kwa karibu na umma na pia Idara ya Polisi (NPS).

“Askari kujifanya mwanahabari ni kukiuka sheria za taaluma. Ni hatari kwa sekta ya uanahabari,” MCK ikasema kupitia taarifa.

Baraza hilo lilitetea huduma za vyombo vya habari na waandishi, likisema wamelindwa na Katiba kupitia Vifungu 33, 34 na 35.

Haki Africa imewataka maafisa wa NPS kukoma kujifanya wanahabari.

 

  • Tags

You can share this post!

Tanzia: Afisa wa serikali ya Kilifi auawa kwa kudungwa kisu...

Kwa kuua waandamanaji polisi wanatekeleza mauaji ya kimbari...

T L