• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
LTWP yajiondolea lawama kupotea kwa stima Ijumaa na Jumamosi

LTWP yajiondolea lawama kupotea kwa stima Ijumaa na Jumamosi

NA CHARLES WASONGA

KITUO cha kuzalisha umeme kutokana na upepo, Lake Turkana Wind Power (LTWP), kimekana madai kuwa hitilafu katika mitambo yake ndio ilisababisha kupotea kwa stima kote nchini Ijumaa.

Stima ilipotea sehemu kadha nchini kwa karibu saa 20 kuanzia Ijumaa hadi Jumomosi, hali iliyosababisha hasara na usumbufu mkubwa kwa Wakenya, haswa wafanyabiashara.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) pia uliathirika, hali iliyochangia Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen kuwapiga kalamu baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA).

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa jioni, kampuni ya Usambazaji Umeme Nchini (Kenya Power) ilidai kuwa hali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika mitambo ya kusambaza stima kutoka kituo cha LTWP, kilicho kaunti ya Marsabit.

Sababu sawa na hiyo ilitolewa na Waziri wa Kawi na Petroli Davis Chirchir kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi mnamo Jumamosi.

Lakini kwenye taarifa, ambayo Taifa Jumapili ilipata nakala yake, kituo cha LTWP kilijiondolea lawama.

“Lake Turkana Wind Power (LTWP) ingependa kufafanua kuwa haikusababisha hali ya kupotea kwa stima iliyokumba nchi Ijumaa na Jumamosi. LTWP ililazimika kuzima mitambo yake ya kuzalisha kawi kufuatia uongezeko la stima katika mtandao wa kitaifa. Tulichukua hatua hii ili kuzuia uharibifu mkubwa,” ikasema taarifa hiyo.

LTWP inasema kuwa hadi wakati ambapo ilizima mitambo yake, mfumo wake ulikuwa ukiwasilisha Megawati 270 za stima katika Mfumo wa Kitaifa (National Grid).

Lakini mnamo Ijumaa Bw Chirchir ambaye alikuwa ameandamana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Power Joseph Siror, aliwaambia wanahabari kuwa tatizo hilo la kupotea kwa stima lilisababishwa na LTWP.

Kwenye taarifa yake, Kenya Power nayo ilisema kuwa kiini cha kupotea kwa stima kilisababishwa na “hitilafu ya kupotea kwa Megawati 270 za stima katika kituo cha Lake Turkana Wind Power (LTWP).”

“Kupotea huko kulisababisha shida katika mfumo wa nguvu za stima hali iliyoathiri vituo vinginevyo na kusababisha kupotea kwa stima,” Kenya Power ikasema.

  • Tags

You can share this post!

Atwoli asifu Rais Ruto kwa ‘kufanya maisha ya Kenya kuwa...

Kidosho wa Kirinyaga aliyeapa ataolewa akiwa milionea akiri...

T L