• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Kidosho wa Kirinyaga aliyeapa ataolewa akiwa milionea akiri ‘alirambwa’ na dalali kibiashara

Kidosho wa Kirinyaga aliyeapa ataolewa akiwa milionea akiri ‘alirambwa’ na dalali kibiashara

NA MWANGI MUIRURI 

KATIKA kisa kinachoelezea jinsi madalali huvuna hela nyingi kutoka kwa wakulima, Julai 5, 2023 Grace Wangechi Kamande 27, alipata wateja wa kijumla kutoka Kaunti ya Nairobi.

Wangechi hukuza mahindi katika shamba la babake Kijiji cha Gatitika, Kaunti ya Kirinyaga na ameapa kuwa ataolewa tu baada ya kuwa milionea katika kilimobiashara.

Kwa kuwa Wangechi hakuwa na ufahamu wa wateja wa jumla, alisajili huduma za David Makui ambaye ni mjanja kivyake na hufanya kazi ya udalali.

Wangechi alikuwa na mahindi mabichi takriban 1, 000 ya kuuza na alikuwa akipania kuuza Sh15 kila moja.

“Lakini dalali wangu aliniambia kwamba bei hiyo ni ya juu sana na hakuna vile wanunuzi wangeikubali kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa bei yao masoko mbalimbali Nairobi,” afichua.

Baada ya mashauriano ya kina, dalali huyo alimuagiza akubali Sh9 ili gharama ya kuvuna, kuipakia kwa gari na uchukuzi pamoja na matumizi ya ushuru na hongo barabarani wateja hao wabakie na faida.

“Nilikubali na nikauza. Aliyelipwa na wateja hao wa Nairobi alikuwa ni Makui. Hakunirusha kwa kuwa alinikabidhi Sh9, 000 tulizokubaliana,” asema.

Lakini baadaye, wateja hao walivutiwa na bidii ya Wangechi na katika gumzo ikafichuka kwamba Makui alikuwa amenunua mahindi hayo kwa Sh9, 000 lakini akayauza kwa wateja hao kwa Sh13 kila moja, hivyo basi kujipa Sh4,000 kama faida.

“Aidha, nilikuja kuelewa kwamba Makui alilipwa Sh2, 500 za ziada kama marupurupu ya kuwaunganisha na mimi kama mkulima, hivyo basi kuzidisha pato lake hadi Sh6, 500,” asema.

Wangechi anasema kwamba yeye faida yake baada ya kuuza mahindi hayo ilikuwa Sh2, 000 pekee.

“Gharama ya kulima shamba, kununua mbegu, mbolea na kunyunyizia maji ambapo nilikuwa nikitegemea vibarua ikiwa ni Sh7, 000,” asema.

Makui aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “Hiyo ndiyo hali ya udalali kwa sasa ambapo sote tunakimbizana na faida”.

Alisema kwamba bora tu hakuna anayetumia mabavu kupata faida, maelewano kati ya mkulima, dalali na mnunuzi ndiyo hali ya mchezo.

“Hata nikiweza kuzidisha faida yangu sitachelea kufanya hivyo…Nilielewana na Wangechi, nikaelewana na wanunuzi na biashara ikatanda huku nikibahatika kuvuna faida kupitia weledi wangu,” asema.

Wangechi alisema kwamba hajachoka kuendelea mbele na harakati zake za kilimo na kile atakachofanya ni kusaka mbinu za kujuana moja kwa moja na wanunuzi.

“Ningekuwa ninajuana na wanunuzi hao wa Nairobi na nishiriki biashara hiyo moja kwa moja, basi ningepata faida ya Sh8, 500 badala ya Sh2, 000 nilizopata,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

LTWP yajiondolea lawama kupotea kwa stima Ijumaa na Jumamosi

Nani walikuwa wamemteka nyara Bwanyenye Singh Rai? 

T L