• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Maafisa waimarisha msako dhidi ya Al-Shabaab baada ya gari la KDF kukanyaga kilipuzi

Maafisa waimarisha msako dhidi ya Al-Shabaab baada ya gari la KDF kukanyaga kilipuzi

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA kadhaa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) wanahofiwa kufariki huku wengine wakijeruhiwa vibaya baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi ambacho inashukiwa kilitegwa ardhini na magaidi wa Al-Shabaab katika Kaunti ya Lamu.

Afisa Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Mawasiliano na Mipangilio jeshini, Brigedia Zipporah Kioko, amethibitishia Taifa Leo Jumatatu kwamba shambulio hilo limetokea eneo la Bodhei-Majengo, kwenye barabara ya Milimani-Baure iliyoko kwenye msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu.

Shambulio hilo lilitekelezwa Jumapili mchana wakati maafisa wa KDF wakiwa kwa gari lao walikuwa wakiendeleza doria zao kama kawaida kwenye eneo hilo ambako kunaendelezwa operesheni ya usalama ndani ya msitu wa Boni.

Operesheni hiyo kwa jina ‘Amani Boni’ ilizinduliwa na serikali kuu tangu Septemba 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwaangamiza au kuwafurusha magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo.

Katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari, Brigedia Kioko alilaani vikali shambulio hilo lililowalenga maafisa wa usalama, akiwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kushinda vita dhidi ya wahalifu, wakiwemo magaidi wa Al-Shabaab.

“Mnamo Septemba 10, 2023, gari la maafisa wetu wa KDF waliokuwa wakishika doria kwenye barabara ya Milimani-Baure lilikanyaga kilipuzi. Waliojeruhiwa tayari wamesafirishwa kwa ndege kwenye kambi ya jeshi ya Manda kwa matibabu. Tunalaani wahalifu wanaotatiza usafiri na masuala ya uchumi na maendeleo eneo hilo. Wananchi mjitokeze kutoa taarifa za kusaidia kukabiliana na adui,” akasema Brigedia Kioko katika ujumbe wake.

Shambulio la Jumapili lililoacha maafisa kadhaa wa KDF wakifariki na wengine kujeruhiwa lilitokea saa chache baada ya mhandisi kujeruhiwa vibaya mgongoni na kichwani kwenye shambulio lingine la kilipuzi kinachoshukiwa kutegwa ardhini na Al-Shabaab kwenye barabara ya Hindi-Bar’goni.

Gari lililokanyaga kilipuzi na kusababisha mhandisi wa Lamu, Hussein Abdi Maali kujeruhiwa mgongoni na kichwani. PICHA | KALUME KAZUNGU

Shambulio hilo lilitekelezwa majira ya saa saba mchana wa Jumamosi.

Eneo la Milimani-Baure ambapo wanajeshi wa KDF walishambuliwa Jumapili liko umbali wa karibu kilomita 60 kutoka Hindi-Bar’goni ambako mhandisi alijeruhiwa Jumamosi.

Kufuatia mashambulio hayo, usalama umeimarishwa vilivyo kwenye barabara ya Hindi-Bar’goni na ile ya Bar’goni-Milimani-Baure-Kiunga.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo Jumatatu mchana wamekiri kuona vifaru vya wanajeshi na magari ya vitengo vingine vya walinda usalama yakipitapita barabarani kuashiria kuwa wameanzisha msako wa kuwakabili magaidi hao.

Kati ya Juni na Septemba 2023, Kaunti ya Lamu imeshuhudia mashambulkio ya kujirudiarudia yanayotekelezwa na Al-Shabaab. Mashambulio hayo yameacha zaidi ya watu 10, wakiwemo maafisa wa usalama wakiuawa huku zaidi ya nyumba 20 ikiwemo kanisa, zikiteketezwa kwa moto.

Baadhi ya vijiji ambavyo vimeathiriwa pakubwa na mashambulio ya Al-Shabaab ni Juhudi, Salama, Widho, Marafa, na Mashogoni.

Mashambulio hayo pia yameacha karibu familia 200 zikitorokea kwenye kambi iliyowekwa katika Shule ya Msingi ya Juhudi iliyoko Lamu Magharibi.

  • Tags

You can share this post!

Polo wa kila mara ‘nionje kidogo’ abugia mkojo...

Gavana wa Nyamira motoni kwa kumfuta kazi Waziri wa Afya

T L