• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 1:47 PM
Polo wa kila mara ‘nionje kidogo’ abugia mkojo akidhani ni pombe 

Polo wa kila mara ‘nionje kidogo’ abugia mkojo akidhani ni pombe 

NA MWANGI MUIRURI

MURANG’A MJINI

POLO mmoja mwingi wa tamaa ya pombe alibugia mkojo nusu glasi baada ya kupangiwa njama ya adhabu mjini hapa.

Kwa mujibu wa mdokezi wetu, polo ambaye ni kibarua mjini amekuwa akiwasinya marafiki kwa kuandamana nao ndani ya baa akiomba aonjeshwe kidogo.

“Hata wakati tunavunja sheria tukiingia ndani ya baa kutoa lock, unampata tu amekufuata. Wakati uko mbioni kuteremsha kinywaji chako kabla polisi wakufumanie, polo ndiye huyo kwa mabega yako akikukumbusha umbakishie kidogo,” akasema mdokezi ambaye pia ni mlevi.

Baada ya kuwakera walevi mtaani hadi kuwafika mwisho, ndipo njama ilipangwa ya kumwadhibu na kumpa adabu za ulevi.

“Walevi walikutana tu na wakampangia njama. Walinunua glasi dukani ya Sh50 na wakafululiza nayo hadi kwa baa moja. Ilikuwa asubuhi saa mbili ambapo baa fulani ilikuwa inatuuzia kinyume na sheria,” akasema mdokezi.

Kwa kuwa mauzo hayo hufanywa katika maeneo fiche ya baa, mara hii karibu na choo siku hiyo, mhudumu alikuwa akiwamiminia pombe ya Sh10, Sh20, Sh50… vipimo kadri ya uwezo wa kila mteja.

“Polo aliingia na akaanza ombaomba zake… Kumbe ‘marafiki’ wake walikuwa wamejaza glasi mkojo wa binadamu na kuiweka kwa sehemu fulani yenye giza karibu na choo,” polo akasema.

Polo alipoomba, akaagizwa achukue glasi moja. Kumbe alichukua hiyo ya mkojo. Hana habari.

“Kwa tamaa kuu mate yakimtoka kwa kasi, polo alikimbia pahala hapo, akapata glasi imejaa pomoni… akaiinua juu kwa furaha na akaiweka mdomoni,” mdokezi asema.

Polo alikuwa amemeza nusu ya glasi wakati aligundua hiyo haikuwa ladha ya pombe.

“Polo alipiga nduru kwa sauti kali mpaka mwenye baa akaamua kufunga mauzo hayo haramu… Alianza kutapika huku akifukuzwa nje. Kwa wiki moja sasa polo hajaonekana mtaani. Ni kama adhabu hiyo imempa adabu za kimsingi kuhusu umuhimu wa kujifadhili uwapo mraibu wa pombe,” akasema mdokezi.

  • Tags

You can share this post!

Jamii yashtuka radi kupiga na kuua mke na mume, kujeruhi...

Maafisa waimarisha msako dhidi ya Al-Shabaab baada ya gari...

T L