• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Madaktari wa binadamu na mifugo watofautiana vikali kuhusu mswada wa kusimamia dawa

Madaktari wa binadamu na mifugo watofautiana vikali kuhusu mswada wa kusimamia dawa

NA MARY WANGARI

MSWADA wa kufanyia marekebisho Sheria inayohusu Mamlaka ya Kusimamia Dawa (KDA) 2022 umeonekana kuwagawanya wataalam kuhusiana na athari za kiafya.

Haya yamejiri kufuatia Mswada mpya kuhusu Kudhibiti Usalama wa Vyakula na Lishe unaolenga kutenganisha sheria zinazosimamia tiba ya binadamu na ile ya mifugo.

Mswada huo uliwasilishwa na Mbunge wa Endebess, Robert Pukose, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya, ukiwa na lengo la kuimarisha usalama wa vyakula kufuatia visa tele vya matatizo ya kiafya yanayotokana na lishe.

Endapo Mswada huo utaidhinishwa na Bunge la Kitaifa, sheria mpya itawezesha bidhaa zinazohusu afya ya wanyama au mifugo kuondolewa chini ya usimamizi wa KDA, hatua inayopingwa vikali na Shirikisho la Wauzaji wa Dawa Nchini (PSK).

“Kuondoa bidhaa zinazohusu afya ya mifugo chini ya usimmaizi wa KDA huenda kukahatarisha afya, bidhaa zinazouzwa katika mataifa ya kigeni na kusababisha kuwepo usimamizi kutoka mamlaka mbili (Kipengele 3, Kifungu 4 cha Ripoti ya PHC ukurasa wa 98 na 140,” ilihoji PSK Jumatatu kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Aidha, wataalam hao wa matibabu ya binadamu wanafafanua kuwa hatua ya “kuwapa leseni maafisa ambao hawana mafunzo ya kutosha inahujumu viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).”

Kwa upande mwingine, hata hivyo, wataalam wa afya ya mifugo wakiongozwa na Muungano wa Madaktari wa Mifugo Nchini (KVA) wameonya kuwa afya ya Wakenya huenda ikahatarishwa pakubwa kutokana na vyakula vyenye sumu vinavyotokana na bidhaa za wanyama, ikiwa Mswada huo hautapitishwa.

Timu hiyo inajumuisha Muungano wa Madaktari wa Mifugo Nchini  (UVPK) Muungano wa Wataalam kuhusu Sayansi ya Mifugo Nchini (KASPA) Muungano wa Wataalam kuhusu  Afya ya Wanyama (AHTTAK) Muungano wa Wataalam kuhusu Afya ya Mifugo (KVPA), na Muungano wa Wataala wa Kiufundi kuhusu Mifugo Afrika Mifugo (AVTA).

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa KVA, Dkt Nicholas Muyale, wataalam wa afya ya mifugo wamekaribisha Mswada kuhusu Usalama wa Vyakula na Lishe wakisema kuwa “bidhaa za matibabu ya mifugo zinasimamiwa kwa njia bora chini ya Wizara iliyotwikwa jukumu la kudhibiti maradhi ya wanyama,” jinsi inavyopendekezwa na Shirika la Afya kuhusu Wanyama Duniani (WOAH).”

Akizungumza na Taifa Leo, Dkt Muyela alifafanua kuwa viwango vya ubora kimataifa vinaagiza kutenganishwa kwa usimamizi unaohusu dawa ya binadamu na dawa ya mifugo.

“WOAH imeweka viwango vya ubora kuhusu afya ya wanyama na dawa ya mifugo. Kifungu 3.4.11 cha Kanuni ya Afya ya Wanyama wanaoishi Nchi Kavu kinapendekeza sheria inayodhibiti uundaji, uuzaji katika nchi za kigeni, uuzaji wa jumla, rejareja, na matumizi ya bidhaa za matibabu ya mifugo kujumuishwa kwenye Mamlaka inayokabiliana na udhibiti wa maradhi ya wanyama,” alisema Dkt Muyela.

Aidha, wataalam hao wameonya kuwa Wakenya huenda wakahatarishwa kiafya iwapo waundasheria watakubali matakwa ya PSK kuhusiana na vipengele vitatu tata kwenye Mswada uliowasilishwa.

“Wataalam wa dawa ya binadamu hawana uwezo au ujuzi wa kuhakikisha usalama wa vyakula. Wataalam wa tiba ya watu wanapaswa kujishughulisha na udhibiti wa dawa ya binadamu ambayo ni chanzo kikuu cha matatizo ya kiafya yanayotokana na uzoefu wa kumeza dawa kiholela,” walihoji kupitia taarifa.

“Mswada wa Kudhibiti Usalama wa Vyakula na Lishe utalainisha mpangilio wa usalama unaohusu vyakula vya biandamu.”

Ikizingatiwa kuwa Kenya imetia saini Mkataba wa WOAH kuhusu Afya ya Wanyama wa Nchi Kavu na Majini kupitia Mikakati ya Mamlaka ya Biashara Ulimwenguni (WTO) kuhusu Usafi (SPS), hatua ya kukosa kutenganisha usimamizi wa tiba ya wanyama na binadamu itaamaanisha imekiuka mkataba huo, wanafafanua.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wa Azimio kususia vikao hadi Sabina avuliwe wadhifa...

Vuguvugu lafika kortini kupiga breki hatua yoyote ya Bunge...

T L