• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Wabunge wa Azimio kususia vikao hadi Sabina avuliwe wadhifa wa naibu kiranja wa wachache

Wabunge wa Azimio kususia vikao hadi Sabina avuliwe wadhifa wa naibu kiranja wa wachache

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wa upinzani sasa wametishia kuvuruga shughuli za bunge juma lijalo ikiwa hatua ya mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya kumwondoa Naibu Kiranja wa Wachache Sabina Chege haitaidhinishwa.

Mnamo Alhamisi alasiri, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alimlaumu Spika Moses Wetang’ula kwa kukataa, kimakusudi, kutekeleza mabadiliko hayo.

Alimsuta Bw Wetang’ula kwa “kuzungusha upinzani na kukataa kutimiza mabadiliko miezi mitano baada ya muungano wa Azimio kufanya uamuzi huo.”

“Ikiwa agizo la mahakama lililotolewa na mahakama mnamo Oktoba 19, 2023, halitatekelezwa na Spika na Mwenje (Mark) aruhusiwe kutekeleza majukumu yake, basi hakuna shughuli zitaendelea katika Bunge la Kitaifa Alhamisi ijayo bunge litakaporejelea vikao vyake,” akasema Wandayi katika kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano.

Akaongeza: “Mwenendo huu wa Spika kutuchezea shere unafaa kukoma kabisa. Wale waliopeleka suala hili kortini sasa wanazunguka huku na kule wakitafuta maagizo mengine kuzuia mabadiliko hayo. Haupaswi kuwa wakili kufahamu mchezo unaoendelea hapa.”

Bw Wandayi ambaye ni mbunge wa Ugunja alisema kuwa upande wa wachache hauwezi kuendesha shughuli zake sawasawa kwa sababu Bi Chege, ambaye ni Mbunge Maalum hauufanyii kazi.

Mnamo Januari 2023 Bi Chege, ambaye aliteuliwa bungeni kwa tiketi ya chama cha Jubilee, aliandamana na wabunge wengine wa chama hicho kumtembelea Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi na kutangaza kuwa watafanya kazi na mrengo wa Kenya Kwanza.

Mnamo Mei 2023, muungano wa Azimio uliamua kumvua Bi Chege wadhifa huo na kumtunuku Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje.

Miezi miwili baadaye, mahakama ya Kiambu ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa mbele yake kupinga kutimuliwa kwa Bi Chege.

Lakini tangu wakati huo, Spika Wetang’ula amejivuta kuidhinisha mabadiliko hayo, hali ambayo imekasirisha wabunge wa Azimio.

Wakati mmoja, wabunge hao walitisha kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Bw Wetang’ula bungeni.

Wiki hii, Bi Chege alitangaza kuwa anapania kuwasilisha kesi katika mahakama ya rufaa kukataa rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Kiambu iliyodinda kubatilisha kutimuliwa kwake.

  • Tags

You can share this post!

Watu sita wapelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa...

Madaktari wa binadamu na mifugo watofautiana vikali kuhusu...

T L