• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Madiwani wa Meru wakerwa na hatua ya Gavana Mwangaza kutaka serikali ivunjwe

Madiwani wa Meru wakerwa na hatua ya Gavana Mwangaza kutaka serikali ivunjwe

Na KEVIN MUTAI

MADIWANI wa Kaunti ya Meru wamekerwa na pendekeza la gavana wa kaunti hiyo Kawira Mwangaza kwamba serikali hiyo ivunjwe na viongozi wote kutafuta viti upya kupitia kwa kura.

Sehemu ya madiwani 59 wanaopinga uongozi wa gavana huyo wanasema kuwa watashughulikia ombi la watu 22 wanaotaka serikali ya kaunti hiyo ivunjwe.

Madiwani hao wanataka kuwasilisha hoja ya kuwatimua afisini mawaziri kadha wa Gavana Mwangaza ili kulemaza serikali yake.

Madiwani hao wako Mombasa kwa warsha ya mafunzo na kujadili masuala kadha yanayowahusu yakiwemo majaribio mawili ya kumng’oa mamlakani gavana wao.

Majaribio ya Taifa Leo ya kupata kauli kutoka kwa madiwani hao yalifeli.

Ni diwani wa wadi ya Abogeta Magharibi Dennis Kiogora alizungumzia suala hilo kwa njia ya simu.

Bw Kiogora akasema: “Raia wako na haki ya kuwasilisha maombi yoyote katika bunge lolote, liwe la kaunti au bunge la kitaifa. Na hauwezi kuwazuia kufanya hivyo, hivyo maombi hayo yakifika mbele yetu tutayashughulikia.”

Upande wa wengi katika bunge la Kaunti ya Meru umetaja hatua ya Bi Mwangaza kushinikiza kuvunjwa kwa serikali hiyo kama ambayo ni ngumu kutekelezwa kwani utaratibu wake ni mrefu.

Madiwani wa mrengo huo wanasema mchakato huo unaweza kudumu kwa miezi mingi mno kutokana na hatua za kisheria na hali kwamba uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haujafanywa.

Mnamo Alhamisi Gavana Mwangaza alisema amepokea mapendekezo kutoka kwa mashirika mbalimbali yanayotaka kuanzisha zoezi la ukusanyaji wa sahihi za kufanikisha kuvunjwa kwa serikali ya Kaunti ya Meru.

“Ikiwa masuala yanayoibua kutoelewana kati ya viongozi hayatatatuliwa, nitaunga mkono pendekezo la kuvunjwa kwa serikali hii,” Gavana Mwangaza akasema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio kinachopeperusha matangazo kwa lugha ya Kimeru.

Kipengele cha 192 cha Katiba kinatoa utaratibu kuhusu njia za kusimamisha kwa muda serikali ya kaunti nchini Kenya.

Aidha, kinasema kuwa Rais anaweza kusimamisha kwa muda serikali ya kaunti kwa sababu mbili; mzozo wa ndani ambao unahujumu utendakazi wake, kulipuka kwa vita au hali nyingi maalum.

Kulingana na kipengele hicho, sharti sahihi zikusanywe kutoka kwa angalau asilimia 10 ya wapiga kura waliosajiliwa katika kaunti husika.

Sahihi hizo sharti zithibitishwe na IEBC.

Baada ya hapo, tume hiyo itawasilisha pendekezo hilo kwa Rais ambaye atabuni tume huru ya uchunguzi kuchunguza madai ya kutaka serikali ya kaunti ivunjwe.

Ikiwa Rais ataridhika kuwa sababu zilizowasilishwa za kutaka kaunti ivunjwe zina mashiko, atawasilisha ripoti katika Seneti ili ijadiliwe na kupitishwa.

“Utaratibu huo unaweza kuchukua muda wa zaidi ya miezi 18 hivi. Huu ni muda mrefu zaidi na ambao utachosha hata wakazi wa Meru,” akasema Bw Kiogora.

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: ‘Kupiga maji’ si sawa na kufyatua choo...

Bei ya juu ya nyanya Kisumu yaumizwa wakazi

T L